Neno La Leo: Kwenye Msafara Wa Gesi Na Mafuta Ya Taa Yamo - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Neno La Leo: Kwenye Msafara Wa Gesi Na Mafuta Ya Taa Yamo

Ndugu zangu,
Nimepata kuandika, kuwa ni heri kufa na kuacha fikra zinazoishi kuliko kuishi bila kufikiri. Na hakuna njaa mbaya kwenye dunia hii kama njaa ya akili. Kwa mwanadamu, ukiwa na shibe ya akili unaweza kumaliza njaa ya tumbo.


Ninachoandika hapa kinakutaka msomaji sio tu ufikiri, bali ufikiri kwa bidii. Kwenye sakata hili la gesi ya Mtwara na Lindi ambayo kimsingi ni gesi ya Watanzania nauona mkanganyiko wa fikra.


Tulipo sasa ni sawa na mwili uliohangaika kubeba mzigo mkubwa, na kusafiri nao umbali mrefu. Mzigo uko begani. Maungo ya mwili yamechoka sana. Safari imekaribia mwisho. Mzigo ukifika sokoni utauzwa kwa shilingi elfu mbili tu. Kitakachopatikana kitakuwa ni faida ya mwili mzima.


Ghafla kichwa kinadai mzigo ubebwe kichwani, na si begani. Na faida itakayopatikana sokoni iwe ni ya kichwa tu. Mikono na mabega imegoma kuinua mzigo kuufikisha kichwani. Kichwa kinasema kiko tayari kumlipa mpagazi atakayesaidia kuufikisha mzigo kichwani.

Gharama ya kumlipa mpagazi ni shilingi mia tano tu. Hivyo, kazi yote iliyofanya mwili kuufikisha mzigo mpaka hatua hii ya safari ni ya bure tu. Kwanza mwili ulichoka, maungo yakalegea. Lakini ghafla, mwili umeanza kuchemka, umekuwa mgumu. Naam, mwili umegoma. Unakataa mzigo usifike sokoni.


Je, kichwa kifanye nini?

Jibu, hakuna jinsi. Kichwa kina lazima ya kukaa chini na kufanya mazungumzo na mwili. Kuna lazima ya kupatikana muafaka, kwa mazungumzo. Hasara ya kichwa na mwili kuingia kwenye mgogoro ni hasara ya wote; kichwa na mwili.


Ndugu zangu,
Kuna ishara mbaya naziona mbele yetu. Maana, sakata hili la gesi ni jambo kubwa na laweza kuwa la hatari pia. Kwenye msafara huu wa hoja ya gesi nayaona mafuta ya taa . Kuna miongoni mwetu, wawe wanasiasa, wanaharakati na hata viongozi wa dini, kwao ya Mtwara na gesi ni ‘ Mtaji katika harakati zao’.


Hata wale Wabunge waliokuwa wakitetea ongezeko la posho zao bungeni sasa wako mstari wa mbele , eti, kuwashawishi Watanzania wa Mtwara kujitenga na kuunda taifa lao. Kama kweli walikuwa na uchungu na wananchi wa Mtwara na Lindi kwanini hawakugoma kuchukua ongezeko la posho zao bungeni? 


Ndugu zangu,

Hii ni nchi yetu. Tunajivunia Tanzania yetu. Kamwe tusizichekee fikra za kihaini za kutaka Watanzania wenzetu wajitenge kutoka kwenye nchi yetu tuliyorithi kutoka kwa mababu zetu. Maana, hatari ya kuzichekea fikra kama hizo ni kupelekea nchi yetu kumegeka vipande vipande.
Kuna haja ya haraka kwa Serikali kutoa elimu kwa umma na si vitisho juu ya hoja hii ya gesi. Vinginevyo itatoa nafasi kwa wachache wenye dhamira ya kupotosha umma wakaendelea kuifanya kazi hiyo.


Chukulia mfano wa mwanasiasa kijana niliyemsikia kwenye taarifa ya habari ya Star Tv hivi majuzi akitamka; kuwa kama gesi ya Mtwara ikichimbwa na kuuzwa yote, Watanzania milioni 45 , kila mmoja atakuwa akikaa tu, na mwisho wa mwezi analipwa mshahara kwa miaka 200!


Lakini mwanasiasa yule kijana alishindwa kuwaambia Watanzania wangelipwa kiasi gani kwa mwezi. Huu ni upotoshaji mkubwa na wa hatari na ndio maana ya kuhitajika jitihada za makusudi za kutoa elimu juu ya suala hili la gesi.


Hoja ya msingi juu ya gesi ya Watanzania iliyogunduliwa Mtwara na Lindi ni kwenye usimamizi na mgawanyo wa faida itakayopatikana kutokana na rasilimali hiyo ili iwanufaishe Watanzania wote, wakiwemo wana Mtwara na Lindi. Kuna hoja za msingi pia juu ya mikataba inayoingiwa baina ya wawekezaji na nchi yetu, kama ina maslahi kwa nchi yetu na watu wake au la.


Naam, kwenye msafara huu wa hoja ya gesi kuna mafuta ya taa pia.

Tukiyadharau, yana uwezo wa kusababisha mlipuko mkubwa utakaoangamiza nchi yetu. Tumeshaziona ishara.
Na hili ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,
0788 111 765

www.mjengwablog.co.tz 

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages