Na Ali Issa-Maelezo Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuongoza Mkutano
wa saba wa Baraza la Biashara Zanzibar utakaofanyika Jumamosi Januari
19 katika ukumbi wa Salama Hoteli Bwawani mjini Zanzibar.
Akitoa taarifa kwa Vyombo vya
habari huko Gulioni katika Jengo la ZSTC Katibu Mtendaji wa Baraza hilo
Ali Haji Vuai alisema mkutano huo wa saba utazikutanisha Sekta za Umma
na Sekta Binafsi, ambao utajadili mada mbili muhimu ambazo ni Maendeleo
ya uwekezaji katika viwanda na Ubiya unaohitajika katika viwanda vya
Zanzibar.
Amesema wameamua kuzungumzia
masuala hayo kutokana na Sekta ya Viwanda Zanzibar kuwa nyuma sana jambo
ambalo pia huchangia ukosefu wa Ajira kwa vijana na mapato kwa
maendeleo ya Zanzibar. Ameongeza kuwa Zanzibar ina fursa
nzuri ya kuanzisha viwanda vipya na kuvifufua vile vilivyokuwepo awali
jambo ambalo litachochea kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi kwa
Zanzibar.
Vuai amefahamisha kuwa Viwanda
vilivyokufa Zanzibar vilitokana na sababu mbalimbali na kwamba Mkutano
huo utakuwa ni sehemu muafaka ya kuelezea chanzo cha kufa viwanda hivyo
na kubuni mipango mipya ya kufufua sekta hiyo. Alisema wamealika wadau
mbalimbali wa Viwanda na Biashara kutoka ndani na nje ya Zanzibar kuja
kujadili namna bora ambapo anaamini kuwa mwisho wa Mkutano huo Zanzibar
inaweza kuja na fikra mpya ya juu ya Viwanda.
Aidha Katibu huyo alisema katika
Mkutano huo Makala tatu zitawasilishwa mbili kutoka katika Sekta ya Umma
na moja itawasilishwa na Sekta binafsi kuhusiana na mambo yanayohusu
njia bora za kuimarisha sekta ya Viwanda Zanzibar. Katibu Vuai pia amewaomba
Wajasiriamali wa Zanzibar kuitumia fursa hiyo adhimu kwao kutangaza
biashara zao kupitia Wageni na wenyeji ambao watashiriki katika mkutano
huo wa Saba toka kuanzishwa Baraza la Biashara la Zanzibar.
Mkutano huo wa siku moja
unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 350 kutoka ndani na nje ya
Zanzibar ambapo Mashirika kama UNIDO, TIDO, TMS, Tume ya Biashara ya
Afrika ya Mashariki ni miongoni mwa waalikwa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)