RUFANI ya kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dar es Salaam (RCO),
Abdallah Zombe na wenzake wanane, inatarajiwa kusikilizwa leo katika
Mahakama ya Rufani.
Hiyo ni baada ya miaka mitatu tangu ilipofunguliwa na inatarajiwa kusikilizwa na Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, linaloundwa na Jaji William Mandia, Jaji Nathalia Kimaro na Jaji Katherine Oriyo.
Katika kesi hiyo, Zombe na wenzake hao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese, Dar es Salaam.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa walikuwa ni Zombe, ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Konstebo Jane Andrew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emmanuel Mabula na Koplo Felix Sedrick,
Wengine walikuwa ni Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Koplo Rashid Lema (aliyefariki kabla ya kujitetea), Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Washtakiwa hao walikuwa wakidaiwa kuwa Januari 14, 2006, katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam, waliwaua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa madini, waliokwenda kuuza madini yao Dar es Salaam na dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha.
Wafanyabiashara hao ni Sabinus Chigumbi, ‘Jongo’ na ndugu yake Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, ambaye alikuwa dereva teksi.
Awali, washtakiwa katika kesi hiyo walikuwa 13, lakini hadi ilipotolewa hukumu, walikuwa wamebakia tisa tu, baada ya wengine watatu kuachiwa huru katika hatua ya awali na mmoja kufariki dunia.
Washtakiwa walioachiwa huru ni Konstebo Leonard, Koplo Moris na Koplo Sedrick walioachiwa huru kabla ya hatua ya kujitetea baada ya kuonekana kuwa hawana kesi ya kujibu.
Pia Koplo Lema, licha ya kuwa miongoni mwa washtakiwa waliopatikana na kesi ya kujibu, alifariki dunia, wakati wenzake wakiwa wameshaanza kujitetea.
Hata hivyo, Agosti 17, 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliwaachia huru washtakiwa wote ikisema kuwa baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote, imeridhika kuwa washtakiwa hawakuwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Hata hivyo, siku chache baada ya kuachiwa huru, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu. Katika rufani hiyo DPP alidai kuwa Jaji Salum Massati aliyetoa hukumu hiyo, alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao kwani kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.
Katika hukumu hiyo, Jaji Massati aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao bila kuacha shaka.
Pia Jaji Massati alisema kuwa amebaini kuwa wauaji halisi hawajafikishwa mahakamani na kwamba kutokana na kutokuwapo kwao mahakamani, mashtaka dhidi ya washtakwa waliokuwapo mahakamani hayawezi kutengenezeka, hivyo akaiagiza Jamhuri kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wauaji halisi.
DPP katika rufaa hiyo namba 254/2009, iliyofunguliwa Oktoba 6, 2009, amebainisha sababu kumi na moja ambazo zimemfanya apinge hukumu hiyo yote, akidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote walikuwa na hatia.
Katika hoja hizo za rufaa, DPP amedokeza kile alichokiita upungufu katika hukumu hiyo, kwa kila mshtakiwa.
Katika rufaa hiyo, DPP katika hoja zake anadai kuwa jaji alipotoka, alishindwa kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu mashtaka ya jinai na kwamba alijichanganya katika hukumu hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)