Mh Zitto Kabwe
.......................................................
Maandamano
ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua
hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na
mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter
na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na
Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA
tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba
udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.
Lakini
kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu
bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha
ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za
CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama
hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM
wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa
Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.
Wanaona
katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu
(kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona
katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM
zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea
kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini?
Watu
wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na
mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe
kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi
yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe
Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi
nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya
Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike
Mtwara tu la hasha.
Sio
dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa
Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa
maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa
nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira?
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini?
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa
kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau
‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu?
Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza
mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara
warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho?
Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za
kigeni baada ya Tumbaku.
Lakini
tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi
fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli
iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali
huru ya Tanzania?
Tujiulize
zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale
Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya
dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu
imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata
ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na
yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana
Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye
Gesi asilia.
Mtwara na Lindi wanakosea wapi?
Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe.
Watu
wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe na
Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha kikundi cha
Watanzania wachache sana. Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa
Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai utajiri
wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi dogo la
watu. Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania wengine
kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho. Watu wa
Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya mnyonge ni
umoja.
Serikali isiyosikia
Serikali
ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa
gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya Watanzania. Kwa
kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa Mtwara wataonekana
hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili kuhusu
mradi huu wa Bomba? Tunaambiwa na Wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa
mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa
imegunduliwa katika Kitalu namba 7( block 7) ambacho kipo mkoani Dar es
Salaam katika Wilaya ya Temeke. Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar
karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa Bomba
unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa na maana tena? Huu mkopo
utakuwa na tija?
Serikali
imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar dhidi ya gharama
za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha umeme kwenda
maeneo mengine ya Tanzania? Serikali imeangalia faida ya kujenga gridi
nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na bwawa la
Mtera? Leo bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja hata Dar es
Salaam izalishe megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo
wa gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa
mgongo Lindi au Mtwara?
Tuwasikilize watu wa Mtwara
Watanzania
sio mabwege tena. Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini, wapuuzi au watu
hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru. Serikali na wadau
wote wa sekta ya Gesi likiwemo Bunge washirikiane na watu wa Mtwara
kuhusu miradi ya gesi asilia. Tuwe na Azimio la Mtwara, tamko la
kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi bila kuathiri umoja
wa Taifa letu.
Ujio wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala
Sasa
hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu nyingine wanahitaji
maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo mbadala wa
kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia raslimali zilizopo na
utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza mfumo wa
kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.
Ni
kwa sababu hiyo naamini chama changu ni jibu sahihi kwa matamanio na
kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe kuwa
katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa
hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika
sera. Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea 2015 na tukishika Dola
wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa
mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa
kushirikiana nao kuleta maendeleo.
Siyo
katika suala la gesi tu bali katika nishati, maji, elimu, miundombinu,
kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa mingine ina
raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha, na zaidi ya
yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. Hili ambalo ni kweli kwa Mtwara
ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi, Lindi n.k.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)