Neno La Leo: Kitendawili Cha Embe Dodo Na Tunakokwenda… - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Neno La Leo: Kitendawili Cha Embe Dodo Na Tunakokwenda…

Ndugu zangu, Jana alasiri pale Bagamoyo nilisimama kununua embe dodo. Akina mama wale wakarimu walinipokea kama mwenzao. Bei ya dodo niliyotajiwa ilinifanya pia nitafakari sana, niingiwe na huzuni pia. 

Maana, ni ukweli, kuwa mama yule anaanza kuzitafuta dodo zinakotoka, kisha anazipanga pale chini mchangani. Bei ya dodo kubwa kabisa ni shilingi mia sita!
Nilinunua dodo saba. Na hesabu ya dodo saba ikampa tabu sana mama yule. Akaniomba nimsaidie hesabu ya haraka. Nikamwambia ni shilingi 4,200. Kwenye noti ya elfu tano niliyompa alihitaji kunirudishia shilingi mia nane. Nikamwambia aitunze chenji hiyo. 

Akashukuru , lakini, wakati akinifungia dodo zangu akaniongeza dodo mbili! Hivyo, kimsingi ameniongeza dodo za thamnani ya 1200! Hivyo, ile mia nane niliyomwachia haina faida kwake. Unafanyaje?

Njiani niliwaza juu ya tunakokwenda kama nchi.Tujiulize; hivi rasilimali zetu za nchi ikiwamo madini, gesi na mafuta tunayoambiwa tunayo kwa wingi yatamsaidia vipi mama yule wa Bagamoyo mwuza embe dodo ambaye yumkini hajui kusoma, kuandika na kuhesabu? 

Na idadi yao inazidi kuongezeka. Takwimu zinasema; asilimia 39 ya Watanzania milioni 45 hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Na hawa wanawaririthisha nini watoto wao?

Kila kizazi na Jukumu Lake; Tafakari,Chukua Jukumu La Kizazi Chako….

 Na hilo Ni Neno 
La Leo.
Maggid Mjengwa,
0788 111 765

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages