Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akisoma hotuba yake ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa pili wa Wanazuoni
wa Bara la Afrika, ulioanza leo katika Ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar
es Salaam.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akipokea zawadi ya Mhe. Rais Jakaya Kikwete, kutoka kwa Kiongozi wa
Umoja wa Wanazuoni, nchini Kuwait, Jasem Mohamed Alitn, baada ya
ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wanazuoni wa Bara la Afrika, ulioanza
leo katika ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya wageni kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika, waliohudhuria
mkutano huo leo, wakimsikiliza Makamu wa Rais, Dkt. Bilal.
Baadhi
ya wageni kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika, waliohudhuria
mkutano huo leo, wakimsikiliza Makamu wa Rais, Dkt. Bilal.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mkutano huo,
baada ya ufunguzi.
*********************************
Makamu
wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amehimiza umuhimu wa kujenga
maelewano mazuri baina ya wafuasi wa dini mbalimbali, vinginevyo, Bara
la Afrika linaweza kushuhudia migogoro ya kidini kama ilivyoanza
kujitokeza huko Nigeria na hata hapa nchini.
Dk.
Bilal ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa
wanawazuoni wa Bara la Afrika uliofanyika katika ukumbi wa Karume, PTA
viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es salaam.
Alielezea
matumaini yake kuwa mkutano huo utayatafakari matukio mbalimbali ya
vurugu za kidini ambazo zimetokea hapa nchini hivi karibuni kwa lengo la
kuweka mustakabali mzuri wa kuishi kwa kuheshimiana baina ya wafuasi wa
dini kuu mbili za Kiislamu na Kikristo.
"Imani
si ugomvi bali imani inapaswa itujenge kimaadili na moja katika tunu za
maadili ni kuishi vizuri na watu wengine hata kama si wa imani yako,"
alibainisha
Makamu
wa Rais alisisitiza umuhimu wa elimu ya mwongozo na ile ya maarifa ya
dunia kwa Waislamu na kusema itawawezesha kutatua matatizo
yanayowakabili wananchi yakiwemo ya uharibifu wa maadili, uasherati,
maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukosefu wa ajira na unyanyasaji wa
kijinsia.
Alitoa
changamoto kwa wanawazuoni wa Kiislamu na viongozi wengine wa dini
kuangalia ni jinsi gani utandawazi hautoathiri imani na maadili ya
waumini lakini pia ni jinsi gani waumini watanufaika na maendeleo
makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyofikiwa na mwanadamu hivi sasa.
Malengo
ya umoja huo wa wanawazuoni Barani Afrika ni pamoja na kutilia nguvu
masuala ya elimu, ushirikiano na kuheshimiana baina ya jamii mbalimbali
Barani Afrika.
Makamu
wa Rais aliyaelezea malengo hayo ni mazuri na ya kujenga ambayo kama
yakiwekwa katika matendo, itaondoa ile picha hasi kuwa waislamu ni watu
wenye kufarakana, wasio na elimu, wasioheshimu dini za wengine na
wasiotambua nafasi na mchango wao katika maendeleo ya nchi hizo.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
Jumamosi – Disemba 15, 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)