Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa maamuzi makali yaliyopelekea kuteua
Kamati ya kusimamia kumaliza mgogoro wa maeneo ya kilimo katika vijiji
vya Dole, Ngurueni na Ndunduke Dole mara baada ya kupokea kero za
Wakulima hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishuhudia nyaraka bandia walizopewa
baadhi ya watu walio nje kabisa ya maeneo ya kilimo ambapo Mkurugenzi
wa Ardhi Nd. January Fusi alizibaini baada ya kuwasilishwa kopi zake na
wakulima hao.Kati
kati ya Balozi Seif na Ndugu January Fusi ni Katibu Mkuu Wizara ya
Kilimo na Mali Asili Zanzibar Nd. Afan Othman aliyevaa kofia ya kiua.
Mwenyekiti wa kufuatilia
matatizo ya wakulima wa Dole na Ngurueni Bwana Daudi Sirus Mukaka
akiwasilisha maazimio yao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif ambayo walikubaliana katika vikao vya awali lakini
hayajatekelezwa na hatiame kuleta kero
Baadhi ya
Wakulima wa Dole, Ndunduke, na Ngurueni Wilaya ya Magharibi wakiwa
katika kikao cha kuwasilisha malalamiko yao ya kucheleweshewa kupewa
umiliki wa maeneo ya kilimo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani hapo skuli ya Wazazi Dole.
--
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imezuia utolewaji wa Hati za umiliki wa maeneo
ya Ardhi kwa ajili ya Kilimo kwa wakulima wa Vijiji vya Dole, Nguruweni
na Ndunduke Dole kufuatia kujichomoza kwa hitilafu za umiliki wa
maeneo hayo kwa baadhi ya watu na kusababisha migogoro kwa kipindi
kirefu.
Uzuiaji
huo umekuja baada ya malalamiko makali yaliyotolewa na Wakulima
hao dhidi ya Watendaji na Maafisa wanaosimamia Ardhi, Kilimo wakiwemo
pia Viongozi wa Ngazi za kati wa Serikali waliyokuwa wakiyawasilisha kwa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Baadhi ya wawakilishi wa Wakulima hao wa Dole, Nguruweni na Ndunduke walimlalamikia
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba tatizo hilo sugu
lilikuwa likichangiwa na baadhi ya maofisa waliopewa jukumuj la
kusimamia maandalizi ya utolewaji wa nyaraka kwa wakulima 28 wa awamu ya kwanza waliokubalika kupatiwa hati ya umiliki huo.
Walisema
Maafisa hao walidiriki kutumia hadaa ya kuchokea majina ya Watu wengine
ambao cha kusikitisha zaidi hawaishi wala kutambuliwa katika maeneo
hayo ya wakulima.
Walalamikaji
hao wa Dole, Ndunduke na Ngurueni walimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba Serikali isisite kuwachukulia hatua kali na za kisheria
watendaji wake wanaoshindwa kutekeleza maagizo ya Viongozi wa juu wa
Serikali.
Walisema tabia hii ya kigugumizi iliyojengeka ndani ya vufua vya baadhi
ya watendaji hao ndio inayochangia kuwapa kiburi kinachosababisha
kujiamulia mambo kinyume na utaratibu kwa kuendeleza ubinafsi zaidi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya
Kilimo na Mali asili Zanzibar Nd. Afan Othman alisema Wizara hiyo
itahakikisha inafanya utaratibu
wa uhakiki wa maeneo hayo ambayo yalikuwa katika umiliki wa Wizara hiyo
kabla ya kumilikishwa kwa Wakulima wa maeneo hayo.
Nd. Afan alisema uhakiki
huo ambao baadhi ya wakulima hao walikuwa wakiuona kero utaiwezesha
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na ile ya Ardhi kuwepuka hitilafu ya
kutokea eneo moja kumilikishwa zaidi ya watu wawili jambao ambalo
linaweza kuzaa mgogoro mwengine mpya usio wa lazima.
Naye Mkurugenzi wa Ardhi Ndugu January Fusi alisema wakati umefika hivi sasa kwa kuiangalia upya sheria
ya umiliki wa ardhi kwa ule utaratibu wa eka tatu tatu waliopewa
wananchi kwa ajili ya kilimo mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
mwaka 1964.
Nd. January Fusi alisema ongezeko
kubwa la idadi ya watu liliopo nchini hivi sasa limesababisha vurumai
kubwa katika umiliki wa ardhi isiyoongezeka ambayo imekuwa mali zaidi
miongoni mwa Wananchi na hata wawekezaji.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema amefikia maamuzi ya kuteua
Kamati Maalum ya Viongozi Wanne watakayosimamia suala hilo na
kulipatia ufumbuzi ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa.
Akishangiriwa
kwa vifijo na makofi na wakulima hao Balozi Seif aliitaja Kamati hiyo
mbele ya wakulima hao kuwa ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
“ Moja kati ya jukumu kubwa la Kamati
hii ni kuhakiki maeneo yote na tufikie hatma ya kuyagawa maeneo haya
kwenu nyinyi wakulima na nisingependa ikapindukia mwishoni mwa mwezi
wa pili mwakani ”.Alifafanua Balozi Seif.
Aliwaeleza
Wakulima hao kwamba ni faraja kwa serikali kuona wananchi walio wengi
hivi sasa wameamuwa kulipa umuhimu unaostahidi suala la Kilimo ambacho
ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwaonya Viongozi na watendaji wenye tabia ya kunyanyasa Wananchi na
hasa wakulima kuacha mara moja mtindo huo ambao unakwenda kinyume na
dhamira na muelekeo wa Serikali.
“ Watu
wanaopewa hati ya umiliki wa maeneo ya ardhi na baadaye kuanza
kunyanyasa wananchi na wakulima waliomo ndani ya maeneo hayo kwa
kuwaamuru waondoke hawafai katika Jamii na inafaa kutengwa kabisa”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Mgogoro
wa maeneo ya ardhi kwa ajili ya Kilimo katika Viji vya Dole, Ngurueni
pamoja na Ndunduke Dole umeibuka tokea mwanzoni mwa miaka 2000 na kuanza
kushughulikiwa na Waziri Kiongozi Mstaafu Mh. Shamsi Vuai Nahodha.
“ Watendaji hawa wanaonekana kubeba
kiburi na kujaa dharau hasa kutokana na kupinga utaratibu ulioridhiwa
na Waziri Kiongozi wa awamu ya Sita wa
kupatiwa hata kama eneo dogo la robo eka pale mkulima anapoendesha
shughuli zake za Kilimo. Lakini chengine cha ajabu hata agizo la Mkuu wa
Mkoa Mjini Magharibi wamelidharau”. Walisema Wakulima hao wakati
wakitoa duku duku lao na huku wakiwaonyeshea vidole baadhi ya viongozi
na watendaji waliochelewesha utaratibu huo.
“Sisi hata kama tutamilikishwa
vijisehemu vidogo vidogo tunavyoendeshea maisha yetu kwa kilimo basi
tutakuwa radhi na kufurahia utaratibu huo utaotupa faraja ya maisha”.
Walisema wakulima hao.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)