Bodi Ya TPDC Yakabidhi Ripoti Kwa Mhe Waziri Wa Nishati Na Madini - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Bodi Ya TPDC Yakabidhi Ripoti Kwa Mhe Waziri Wa Nishati Na Madini

Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Profesa Sospeter Muhongo akikabidhiwa taarifa kuhusu mikataba iliyokwishaingiwa na Serikali ya Utafutaji mafuta na gesi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Michael Mwanda
Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Profesa Sospeter Muhongo akipitia taarifa kuhusu mikataba iliyokwishaingiwa na Serikali ya Utafutaji mafuta na gesi mara baada ya kuipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Michael Mwanda.
 
Na: Afisa habari, Wizara ya Nishati na Madini
 
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imekabidhi rasmi kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ripoti kuhusu mikataba iliyokwishaingiwa na Serikali ya utafutaji mafuta na gesi asilia. Ripoti hiyo ilikabidhiwa Ijumaa iliyopita, Novemba 30 mwaka huu ofisini kwa Waziri jijini Dar es Salaam.

Ripoti hiyo iliandaliwa kufuatia agizo la Mhe. Waziri kwa Bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asilia. Lengo mahsusi lilikuwa ni kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya baadaye, pamoja na kuwezesha Bodi hiyo kuelewa vizuri kazi iliyo mbele yao.

Akipokea ripoti husika kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi Bw. Michael Mwanda, Waziri Muhongo aliahidi kuisoma na kuyafanyia kazi mapema mapendekezo yote. Aidha, aliipongeza Bodi hiyo kwa kufanya kazi hiyo na kuwasilisha kwa wakati akisisitiza kuwa suala la kujali muda ni moja ya mambo ya msingi anayoyasimamia ili kuwa na utekelezaji makini wa majukumu mbalimbali hususan katika Wizara anayoiongoza.

Waziri Muhongo pia alisema ni vyema kwa Wajumbe wa Bodi wakajifunza kwa haraka kutoka nchi zilizofanikiwa kutokana na rasilimali za mafuta na gesi asili, kama Uholanzi, Oman, Malaysia na Norway.

Kwa upande mwingine alisema ni vyema pia kujifunza kutoka nchi ambazo hazijafanikiwa katika kusimamia rasilimali husika kama Nigeria ili kupata ufahamu wa makosa waliyofanya ambapo ufahamu huo utawasaidia kuepuka makosa ambayo nchi hiyo ilifanya.

Aidha, Serikali inaandaa Sera ya gesi asili kwa umakini ili iwe dira ya kuongoza shughuli za uzalishaji na utumiaji wa gesi asili. Mikataba 26 ya TPDC ni sehemu ya nyaraka muhimu za kuboresha utayarishaji wa sera ya gesi asili. Wananchi wote wanahusishwa kutoa maoni ili kuiboresha Sera hiyo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages