Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali wakifuatilia mada anuai katika tamasha hilo
Na Mwandishi wa Thehabari.com, Mkambarani-Morogoro
TAMASHA la Jinsia Ngazi ya Wilaya linalofanyika
Kijiji cha Mkambarani-Morogoro limeanza rasmi kwa kufunguliwa kwa
mjadala wa wazi uliotoa nafasi kwa washiriki kushirikishana maswala
anuai ya kijamii. Mada Kuu ya tamasha hilo inasema; ‘Haki ya Uchumi, Rasilimali
Ziwanufaishe Wanawake Walioko Pembezoni. Tamasha hilo linaendelea kwa
siku tatu mfululizo nje kidogo ya Mji wa Morogoro, eneo la
Moseka-Mkambarani, ambapo wananchi mbalimbali pamoja na wanaharakati
ngazi ya jamii wanahudhuria kuchangia mada mbalimbali zinazotolewa eneo
hilo.
Masuala yaliyoibuka kwa mkutano wa jana ni pamoja na migogoro ya
ardhi kati ya wananchi na wanakijiji wa eneo la Mkambarani dhidi ya
wawekezaji wanaoingia kutaka kuwekeza hasa kwenye mashamba.
Baadhi ya wananchi wameomba viongozi wa juu kuingilia mgogoro wa
ardhi uliopo kati ya wananchi na taasisi ya Islamic Foundation, ambapo
inadaiwa wananchi kuyaachia mashamba yao waliyokuwa wakilima awali ili
yachukuliwe na taasisi hiyo. Wananchi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wameomba zifuatwe
taratibu kama kuna wawekezaji wanataka kuingia kwenye ardhi ya
wanakijiji ili mazungumzo yafanywe na Serikali ya kijiji na si
vinginevyo. Mkutano huo unaendelea tena leo na unatarajia kufikia kikomo
Ijumaa ya wiki hii.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)