1.0 Utangulizi
Mtihani
wa Taifa wa Kidato cha Pili mwaka 2012 unatarajiwa kufanyika nchini kote
kuanzia tarehe 05/11/2012 na kumalizika tarehe 16/11/2012. Idadi ya
shule/vituo vilivyosajili watahiniwa mwaka 2012 ni 4,242 ikiwa ni
ongezeko la vituo 55 ikilinganishwa na vile vilivyosajiliwa mwaka 2011
ambavyo vilikuwa 4,187. Kwa hiyo kwa mwaka huu kuna ongezeko la asilimia
1.3.
2.0 Watahiniwa
Jumla ya
watahiniwa 442,925 wamejiandikisha kufanya mtihani. Kati yao wasichana
ni 214,325 (sawa na asilimia 48.39) na wavulana ni 228,600 (sawa na
asilimia 51.61).
3.0 Umuhimu wa Mtihani wa Kidato cha Pili
Mtihani
wa Kidato cha Pili kama ilivyo mitihani mingine ya taifa ni muhimu
sana. Matokeo ya mtihani huu hutumiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania
kama sehemu ya matokeo katika mtihani wa taifa wa elimu ya sekondari
kidato cha nne. Mwaka huu, 2012 matokeo ya mtihani huu pia yatatumika
kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa
watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Aidha,
mtahiniwa ataruhusiwa kukariri Kidato cha pili mara moja tu na endapo
mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia,
itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
4.0 Hitimisho
Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaagiza Wadau wote wa Elimu katika Kanda,
Manispaa na Halmashauri za Wilaya pamoja na Wazazi kuhakikisha kuwa
wanafunzi wote walioandikishwa kufanya mtihani wanafanya bila kukosa.
Aidha,
Wazazi, Walezi, Walimu na jamii kwa ujumla wanashauriwa kuwaandaa vema
wanafunzi ili kuepukana na udanganyifu ikiwa ni pamoja na kuzingatia
taratibu na sheria za uendeshaji wa mitihani.
Nawatakia watahiniwa wote wa Kidato cha pili mwaka huu mafanikio mema katika mitihani yao.
Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb)
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
04/11/2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)