Baada ya miezi mitatu ya mchuano mkali hatimaye mshindi
wa shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search atapatikana leo katika
fainali kali inayofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Mshindi atajinyakulia shilingi milioni hamsini pamoja
na mkataba wa kurekodi kutoka kwa wadhamini pekee wa shindano hilo kampuni
ya simu za mikononi ya Zantel.
Washiriki walioingia kwenye fainali hizo ni EBSS06:
Nsami Nkwabi, EBSS07: Nshoma Ng’hangasamala, EBSS09: Salma Abushiri,
EBSS11: Wababa Mtuka (Dar) na EBSS12: Walter Chilambo (Dar).
Wasanii watakaoburudisha ni Rich Mavoko, Omi Dimpoz,
Ben Paul, Lina, Amini, Mzee Yusuf, Haji Ramadhan, Mwasiti, Ditto, Laila
Rashid, Linex na Barnaba.
Akizungumzia fainali hizo, jaji mkuu wa shindano
hilo, Madam Ritha Paulsen, aliwashukuru watanzania kwa ushirikiano waliowapa
toka shindano limeanza mpaka leo wanahitimisha kwa fainali.
‘Kama mlivyoona shindano hili toka lilipoanza
mwaka huu limekuwa la kimataifa zaidi, hivyo tarajieni fainali za kipekee
na zitakazoweka rekodi kwenye tasnia ya burudani na ni matarajio yetu
kwamba mshindi wa usiku huu atafanya vizuri kwenye muziki’ alisema
Madam Ritha.
Kwa upande wake Afsa Biashara mkuu wa Zantel, bwana
Sajid Khan alisisitiza utayari wa kampuni yake katika kuwaendeleza vijana
wa kitanzania kufikia ndoto zao lakini aliomba pia wadau wengine wa
sanaa kuwapa washirikiano washiriki wote.
‘Zantel, pamoja na kumpa mshindi zawadi ya milioni
hamsini lakini pia tutampa mkataba wa kurekodi, na washiriki wengine
watapewa nafasi ya kurekodi wimbo mmoja mmoja lakini juhudi hizi zitafanikiwa
ikiwa tutapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau’ alisema Khan.
Shindano hilo limekuwa likirushwa hewani na kituo
cha runinga cha ITV, lilianza mwezi wa sita kwa kufanya usaili mikoani,
ambalo mwaka huu lilienda mikoa nane-Mbeya, Dodoma, Mwanza, Tanga, Dar
es Salaam, Zanzibar, Lindi pamoja na Arusha.
Kwa mara ya kwanza pia shindano hilo liliweza kufanya
usaili kwa njia ya simu ili kuwapa nafasi vijana zaidi ambao hawakufikiwa
na majaji.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)