kunani msimbazi???? - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

kunani msimbazi????



Na Mwandishi maalum
Nongwa na mgomo baridi unaofanywa na wachezaji wazalendo wa Simba inatokana na uwiano usio sawa wa mishahara baina yao na wachezaji  wageni, kiasi hata  timu hiyo kuboronga katika mechi zake za ligi kuu ya Tanzania Bara.

Uchunguzi umebaini kuwa, baadhi ya wanasoka wazalendo hawafurahii wenzao wa kigeni kulipwa mishahara minono wakati mchango wao katika timu ni mdogo.
Uchunguzi huo umegundua kuwa, hali hiyo imewafanya wachezaji hao wacheze chini ya kiwango kwa lengo la kuushinikiza uongozi kuweka uwiano mzuri wa mishahara.
Mchezaji mmoja mwandamizi wa timu hiyo, alitoa mfano wa wachezaji kama Komabil Keita na Paschal Ochieng, ambao alidai wanalipwa mshahara wa shilingi milioni 1.5 kwa mwezi, lakini wamecheza idadi ndogo ya mechi hadi sasa.


Mchezaji huyo alisema kuwa, viwango vya mishahara kwa wachezaji wazalendo ni kati ya shilingi laki tano na milioni moja wakati kiwango cha juu kwa wanasoka wageni ni shilingi milioni tatu. Felix Sunzu, raia wa Zambia ndiye mchezaji ghali kuliko wote katika klabu ya Simba akiwa analipwa mshahara wa shilingi milioni tatu wakati Mganda Emmanuel Okwi naye amekuwa akishinikiza kuongezwa mshahara katika mkataba wake mpya.
Kwa sasa, Okwi anaramba shilingi milioni 1.5. Wachezaji, ambao wamekuwa wakitajwa kulipwa kiwango kidogo cha mshahara wakati mchango wao ni mkubwa katika timu ni pamoja na Shomari Kapombe, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Nassor Masoud 'Cholo'. Mrisho Ngasa, ambaye amesajiliwa na Simba akitokea Azam, analipwa mshahara wa shilingi milioni mbili wakati Kapombe anakunja shilingi laki saba baada ya kupandishiwa hivi karibuni kutoka shilingi laki tano.
Kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, mgomo huo ndio uliosababisha Simba ilazimishwe kutoka sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro kabla ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, na juzi Jumamosi kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Toto African katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam .
Alipoulizwa, kiongozi mmoja wa Simba alikiri kutambua kuwepo kwa mgomo huo na kuongeza kuwa, wanatarajia kukutana hivi karibuni kujadili hatua za kuwachukulia wachezaji wanaowashawishi wenzao kucheza chini ya kiwango.
Simba, ilianza ligi kuu kwa kishindo na ushindi wa mfululizo, lakini katika siku za hivi karibuni imekuwa ikidorora na kujikuta ikimaliza mzunguko wa kwanza ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Azam na Yanga, na kuchafua rekodi yake kwa kupoteza michezo miwili, dhidi ya Mtibwa na Toto African.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages