Na Mwandishi wetu
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaagiza viongozi wa Mashirikisho ya
sanaa hapa nchini kufuatilia kwa karibu matukio ya ukiukwaji wa maadili
yanayoendelea katika Sanaa hivi sasa na kuchukua hatua kwa wnaobainika
kufanya hivyo.
Katibu
Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego, mbali na BASATA kuwakemea vikali
wasanii wanaotumia majukwaa kwa kuidhalilisha Sanaa wao wenyewe na
watazamaji pia limeyataka mshirikisho kushirikiana na vyama vyao kuwaita
wale wote watakaohusika na uvunjwaji wa maadili ili kuwakanya katika
hatua ya kwanza na kama wasipoacha tabia hizo Baraza litawafungia
kujishughulisha na kazi ya Sanaa hapa nchini.
“Shirikisho
la Muziki tumeliagiza kuangalia tungo za wanamuziki zenye maneno yenye
lugha isiyofaa, Shirikisho la Sanaa za Ufundi limeagizwa kuwachukulia
hatua wasanii wachoraji na wachongaji wanaotengeneza Sanaa zinazokiuka
maadili. Aidha Shirikisho la Sanaa za Maonyesho waliagizwa kufuatilia
wasanii wote wanaocheza bila staha majukwaani. Na mwisho Shirikisho la
Filamu tumeliagiza kuwaita, kuwaonya na kuwachukulia hatua wasanii wote
katika fani ya Filamu wanaovaa nusu utupu bila kuzingatia husika katika
kazi za Sanaa,” amesema Ghonche.
Aidha
Baraza limewaagiza wamiliki wa kumbi zote za burudani kuzingatia
maadili pale ambapo Sanaa zitakuwepo jukwaani na kwamba baraza
halitasita kuufungia ukumbi wowote utakaokiuka agizo hilo.
“Pia
tunaviomba vyombo vya usalama kuhakiki muda wa vibali vya maonyesho na
bila kuchelewa kuwachukulia hatua stahiki wasiozingatia muda wa
maonyesho. Na tunawakumbusha wamiliki wa vyombo vya Habari na Wahariri
kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wasimamizi wa sanaa kwa kutokurusha
wala kutangaza maonyesho ambayo kwa njia yoyote yanachangia mmomonyoko
wa maadili ya Taifa letu,” alisema Ghinche.
Kwa
suala hili, Baraza linaziomba mamlaka zinazohusika na usimamizi wa
uendeshaji wa vyombo vya habari nchini kuingilia kati na kuvichukulia
hatua vyombo vya habari ambavyo kila siku vimekuwa mstari wa mbele
kueneza wimbi la mmomonyoko wa maadili hapa nchini na kushusha hadhi ya
Tasnia/Sekta ya Sanaa nchini.
Sanaa ni kazi na Sanaa ni kioo cha Jamii.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)