Rais Jakaya Kikwete Ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada akianzia mjini New York - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Rais Jakaya Kikwete Ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada akianzia mjini New York

 Rais Jakaya Kikwete
--
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anaanza Ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada akianzia mjini New York, Marekani leo,Jumatatu, Oktoba Mosi, 2012.

Rais Kikwete na ujumbe wake uliondoka nchini usiku wa jana, Jumapili, Septemba 30, 2012, na utawasili mjini New York, Marekani mchana wa leo tayari kwa ziara hiyo ya Marekani. Rais Kikwete atakuwa Marekani kwa siku mbili kabla ya kwenda Canada kwa ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili.


Katika ziara yake mjini New York, Marekani, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon ofisini kwa Katibu Mkuu huyo kesho asubuhi Oktoba 2, 2012.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete ataungana na Mheshimiwa Ban Ki Moon, Meya wa Jiji la New York na Mfadhili Mkubwa wa Misaada yaKibinadamu Duniani, Mheshimiwa Michael Bloomberg; Mama Helen Agerup ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Misaada ya Kibinadamu ya H&B Agerup na Dkt. Kelly J. Henning, Mkurugenzi wa Mipango ya Sekta ya Afya ya Taasisi ya Bloomberg Philanthropies kwenye Uzinduzi wa Matokeo ya Mpango ya Ubunifu wa Afya ya Akinamama katika Tanzania.


Kwenye sherehe hiyo iliyopangwa kufanyika kwenye ukumbi uitwao Green Room kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete, Mheshimiwa Ban Ki Moon, Meya Bloomberg na mama Helen Agerup kwa pamoja watazindua Matokeo ya Mpango huu uitwao Innovative Maternal Health Program.


Kwenye shughuli hiyo pia Meya Bloomberg atatangaza matokeo ya miaka mitatu ya misaada ya kiafya chini ya mpango huo kwa akinamama iliyotolewa na taasisi ya inayomilikiwa na Meya Bloomberg ya Bloomberg Philanthropies Aidha, kwenye shughuli hiyo, Meya Bloomberg atatangaza misaada mpya wa mabilioni ya fedha kuboresha afya ya akinamama katika Tanzania chini ya mpango huo na atatangaza mshirika mpya ambaye atasaidiana na taasisi ya Bloomberg Philanthropies katika kuunga mkono huduma bora za afya kwa akinamama wa Tanzania.


Katika Tanzania, misaada ya taasisi ya Bloomberg Philanthropies huelekezwa katika maeneo ya vijijini yasiyokuwa na huduma bora zaidi kwa kiafya na huduma ambazo hutolewa ni zile za kuokoa maisha ya akina mama hasa wakati wa uzazi.


Tokea mwaka 2006, taasisi hiyo imetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 11.5 Fedha hizo ni sehemu ya kiasi cha dola za Marekani milioni 330 ambazo zilitolewa na taasisi hiyo kwa nchi mbali mbali duniani kwa mwaka jana peke yake.


Taasisi hiyo hufanya kazi ya kuendeleza maeneo matano duniani ambayo ni Usanii, Elimu, Mazingira, Ubunifu katika Serikali na Afya ya Umma.

Rais Kikwete ataondoka Marekani kwenda Canada keshokutwa Jumatano Oktoba 3, 2012 kwa ajili ya Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika nchi hiyo kwa mwaliko wa Gavana Jenerali wa nchi hiyo, Mheshimiwa David Johnston.



Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.

Dar es Salaam.

1 Oktoba, 2012

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages