PICHA ZAIDI WAKATI SHEIKH PONDA NA WAFUASI WAKE WALIPOFIKISHWA MAHAKAMANI JANA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

PICHA ZAIDI WAKATI SHEIKH PONDA NA WAFUASI WAKE WALIPOFIKISHWA MAHAKAMANI JANA

 Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda (mwenye kanzu) akiwa chini ya ulinzi wa askari wakati akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es salaam baada ya kusomewa mashtaka ya wizi, uvunjifu wa amani na uchochezi.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda akishuka katika gari lililomleta katika Mahakama ya Kisutu jana
 Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa (mwenye kanzu nyeupe mbele) akiwa katiika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alikofikishwa pamoja na wafuasi wanaomuunga mkono kama wanavyoonekana pichani.
Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa (mwenye kanzu nyeupe mbele) akiwa katiika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
 Hali ya ulinzi ilikuwa kama inavyoonekana, ambapo askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wakilinda amani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
 Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakitawanyika baada ya Sheikh Ponda na wafuasi wake kurejeshwa mahabusu. 
Sheikh Ponda akipanda gari kurejea mahabusu. Picha zote na Habari Mseto Blog.
 
DAR ES SALAAM, Tanzania
 
KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, na wafuasi wake 49 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijiji hapa leo mchana,
kwa kosa la uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Shilingi milioni 59.

Sheikh Ponda wanaoshitakiwa pia uvamizi wa kiwanja namba 311/2/4 kilichoko Block T Chang’ombe ambacho ni mali ya Kampuni ya Agritanza,   wanatetewa na wakili wa kujitegemea Nassor Mansoor.

Wakati wakifikishwa na baadaye  kuondoka kwenye viwanja vya mahakama hiyo wakiwa ndani ya magari ya Polisi na Jeshi la Magereza, walikuwa wakisikika wakipaza sauti wakisema; ‘Allah Akbar, Allah Akbar’.
 
Sheikh Ponda pia amefikishwa mahakamani hapo akidaiwa kuwashawishi Waislamu kugomea zoezi la sensa ya watu na makazi, iliyofanyika mwezi uliopita nchini kote na kufanya zoezi hilo kufanyika kwa kusuasua.

Hali ya usalama kwenye mahakama ya Kisutu na maeneo ya jirani iliimarishwa mchana wa leo, wakati Sheikh Ponda aliyekamatwa jana na Jeshi la Polisi na kufikishwa Makao Makuu ya Jeshi hilo katikati ya jiji – akifikishwa hapo na Waislamu wengine walioshiriki uvamizi wa kiwanja Chang’ombe.

Baada ya kukamatwa juzi usiku na kufikishwa Kituo Kiuu cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya Waislamu wanaomuunga mkono walivamia kituoni hapo kushinikiza kuachiwa kwa kiongozi wao, kabla ya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Hali ya amani imekuwa tata nchini katika siku za karibu, tangu Ijumaa iliyopita, ambapo kundi la watu wanaosadikika kuwa ni Waislamu walivamia kituo cha polisi huko Mbagala Zakhiem wakishinikiza wakabidhiwe kijana aliyedaiwa kukojolea Msahafu.

Baada ya kushindwa kufanikisha azma hiyo, hasira zao zikaishia katika uvamizi wa makanisa, ambayo kadhaa yalichomwa moto, kuharibiwa na kuibiwa kwa vitu mbalimbali na polisi kuwakamata watu zaidi ya 120 kabla ya kuchujwa na kubaki 36 waliofikishwa mahakamani.

Hali haikuwa shwari pia Visiwani Zanzibar, ambako kikundi maarufu cha Uamsho kimefanya vurugu jana, wakimskaka kiongozi wao mkuu Sheikh Farid, aliyedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana juzi usiku.

Kesi ya Sheikh Ponda ambaye alinyimwa dhamana na wenzake itatajwa tena Novemba Mosi mwaka huu, ambapo watarudi mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages