Nauli za treni Dar es Salaam ni 400/- kwa 500/- - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Nauli za treni Dar es Salaam ni 400/- kwa 500/-


USAFIRI wa treni ndani ya jiji la Dar es Salaam unaanza rasmi kesho huku Serikali ikiwa imetoa msimamo wa nauli zitakazotozwa kwa safari moja kuwa ni Sh 400 kwa reli ya Kati na Sh 500 kwa ya Tazara

Msimamo huo umetokana na uamuzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kupunguza kati ya Sh 200 na Sh 300 kutoka katika nauli zilizopendekezwa awali na waendesha huduma ya usafiri huo ambazo ni Sh 700 kwa treni ya Kati na Sh 800 kwa ya TAZARA.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba alisema, nauli kwa wanafunzi ni Sh 100 na kwamba nauli hizo hazitazingatia endapo msafiri anashuka katikati ya safari au mwisho, hadi utaratibu wa kuweka tofauti ya nauli kulingana na umbali, utakapokamilika.

“SUMATRA ni chombo cha Serikali sasa kilifanya kazi nzuri ya kupitia mapendekezo ya waendesha huduma hiyo ya reli yaliyotaka nauli iwe Sh 700 kwa TRL na Sh 800 kwa TAZARA, pamoja na maoni ya wadau wa usafiri huo waliotaka watozwe Sh 300 na 350 kwa njia hizo...”.

“Baada ya kupitia mapendekezo ya pande zote mbili, iliamuliwa nauli ziwe kama nilivyotaja, sasa kwa kuwa SUMATRA ni chombo chetu, tunautangaza uamuzi huo kuwa ndio msimamo wa Serikali,” Tizeba alisema.

Kuhusu vituo vya kuuzia tiketi, Tizeba alisema vipo zaidi ya 2,000. Sambamba na hilo, alisema, patakuwa na wahudumu (ma-TT) watakaokuwepo milangoni kukagua tiketi, hivyo wasafiri wasithubutu kuleta vurugu kwa kuingia garini bila tiketi, kwa kuwa hatua zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema, kwa kuanzia kutakuwa na treni moja kwa TRL na moja kwa TAZARA zitakazofanya kazi kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi saa 5:00 asubuhi ambazo zitapumzika na kuanza tena safari saa 9:00 alasiri hadi saa 2:00 usiku, kwa siku saba za wiki.

Wakati huo huo, Tizeba alitaja vituo vitakavyotumiwa na treni ya TRL kuwa ni stesheni ya katikati ya jiji, Kamata, Buguruni, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata Matumbi, Tabata Mwananchi, Mabibo na Ubungo Maziwa.

“Kutakuwa na vituo 10 katika reli ya TAZARA itakayoanzia kwenye stesheni yake ya Dar es Salaam hadi Mwakanga. Na kwa safari zinazoishia Kurasini, kutakuwa na vituo vinane,” alisema.

CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages