Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisoma Hotuba ya kufunga Mkutano
wa Tisa wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa aukifanyika katika
Ukumbi wake uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Spika wa Baraza
la Wawakilishi Mh. Pandu Ameir Kificho akiwa na Makatibu wake wakitoka
nje ya Ukumbi wa Baraza hilo baada ya kuahirisha Kikao cha Baraza hilo
Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mwakilishi wa
Jimbo la Kikwajuni Mh. Mahmoud Mohammed Mussa mara baada ya kubaliza
Hotuba yake ya kufunga mkutano wa Tisa wa Baraza la Wawakilishi
Mwakilishi wa
Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza Hassan akibadilishana mawazo na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kufungwa kwa
mkutano wa Tisa wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar
---
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamuonea haya wala kumuogopa mtu ye yote ambae atabainika kuhusika na uvunjifu wa amani baada ya Seriikali kuvumilia vya kutosha, uvumilivu ambao umefikia kikomo.
Kauli hiyo imetolea
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati
akiufunga mkutano wa Tisa wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema
Serikali kupitia vyombo vya ulinzi itaendelea kuvisaka vikundi vya
kihuni vinavyoendesha vitendo vya kuwatisha Wananchi na kuwanyang’anya
vitu na mali zao, kuchoma moto baadhi ya Majengo sambamba na kuharibu
miundo mbinu ya Bara bara.
Alisema hali
hiyo ya vurugu sio Utamaduni wa Wananchi wa Visiwa hivyi ambayo ni ya
kusikitisha iliyopelekea wananchi kuacha shughuli zao za kujitafutia
riziki kutokana na kusimama kwa harakati zao za maendeleo
“ Tutafanya kosa kubwa
sana ikiwa tutaanza kuichezea amani tuliyonayo kwani kuvunjika kwa
amani Nchini mwetu ndio chanzo cha kuvunjika kwa Umoja wetu.”
Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwanasihi
Wananchi kuacha kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani kwani
kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali haitasita
kumchukulia hatua mtu ye yote atakayejihusisha na vitendo hivyo.
Aidha Balozi Seif
aliwaomba Wananchi kutoa Taarifa kwa vyombo vya dola mara tu watakapoona
dalili za watu wenye nia ya kutaka kufanya vitendo vya uvunjifu wa
amani.
Akizungumzia suala
la Rushwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema
Serikali inaendelea kuchukuwa hatua za kuimarisha Taasisi za kupambana
na Rushwa.
Alisema Viongozi pamoja na Wananchi wana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa Taasisi ya kupambana na Rushwa iliyopitishwa na Baraza hilo hivi karibuni ili iweze kutekeleza majukumu na wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kwa kwa faida ya maendeleo ya Taifa.
“ Kama sote
tunavyojua rushwa ni adui wa haki na hivyo haina budi kupigwa vita ili
itokomezwe kabisa. Lakini hizi hazitafanikiwa bila ya ushirikiano wa
wananchi wenyewe”. Alifafanua Balozi Seif.
Kuhusu kundi la
watu wenye Ulemavu Balozi Seif alisema Serikali imeweka mikakati katika
kujenga usawa na kuheshimu haki za watu wote wenye ulemavu.
Alieleza kwamba
kuwapatia watu wenye nulemavu haki zao za msingi ni jambo la Kikatiba na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha azma hii inafikia
malengo yaliyowekwa.
Balozi Seif
aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi
kubwa inayochukuwa katika kuimarisha mazingira kwa watu wenye ulemavu na
kuwajengea uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.
Akigusia suala la
tume ya kukusanya na kuratibu Maoni ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano
Balozi Seif aliwaomba Wananchi ambao bado hawajatoa maoni yao kuitumia
fursa hiyo itakayoamua mambo muhimu yatakayokuwa na maslahi kwa Jamii
yetu.
Alisema si vyema
kwa baadhi ya vikundi vya Wananchi kuiacha fursa hii na kuendelea kutoa
matamshi yanayochochea nchuki, uhasama na vurugu kwa kisingizio cha
kuukataa Muungano.
ASlisisitiza kwamba jambo la kubwa
la kuzingatia ni kuitumia fursa hii ili Wananchi wote waweze kuitoa
maoni yao kwa uhuru bila ya kubughudhiwa na kutishiwa maisha yao.
Kuhusu Sekta ya Umeme Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema
suala la mgao wa umeme karibu litakuwa historia katika Kisiwa cha
Unguja kufuatia kutandikwa kwa waya mpya wa umeme wenye uwezo wa
kuchukuwa umeme wa Mega Watts 100 kazi ambayo inatarajiwa kukamilika
mwezi Disema mwaka huu wa 2012.
Alisema hatua hii
ni faraja kubwa kwa Wananchi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba umeme
ndio nishati muhimu kwa shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa
hili.
Aliwataka Wananchi
wote waendelee kuitumia nishati ya umeme kwa shughuli zao za kujiajiri
kwa nia ya kujikomboa kutoka kwenye umaskini.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi jumatano ya Tarehe 16 Januari mwaka 2013 saa 3.00 za Asubuhi.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)