Moja ya hadithi za Mtume
Muhammad S.A. W ni pale Mtume Muhammad alipokuwa msikitini na maswahaba
wake. Mara akaingia msikitini mtu wa kabila la Mabedui na kuanza
kukojoa. Maswahaba wa Mtume wakasimama kwa hamaki kutaka kumwadhibu
Bedui yule.
Mtume akawasihi maswahaba wake
wasifanye jambo lolote litakalomdhuru Bedui yule. Hapo ikavutwa subira.
Bedui yule akakojoa na akamaliza. Mtume Muhammad alipomuhoji Bedui yule
ikabainika kuwa alikuwa ni mtu wa hovyo na wala hakujua kuwa alimokuwa
ni msikitini. Bedui yule akaelimishwa, akaelewa. Akarudi kwenye
ustaarabu.
Ndio mkojo ule ulifutwa kwa maji
na amani ikawepo. Wahenga walinena; Subira yavuta heri. Siku zote,
hamaki si jambo jema. Kwa kutanguliza subira na kutumia hekima Mtume
Muhammad aliivuta heri na kuepusha shari.
Maana, kama Mtume alisingewaasa
maswahaba wake kuvuta subira, basi, makubwa matatu yangetokea ndani ya
msikiti ule; Mosi, zingezuka vurugu na watu kuumizana na hata kutoana
roho. Pili, mkojo wa Bedui yule ungesambaa msikitini kwa vile alishaanza
kukojoa na isingekuwa rahisi kwake kukatisha mkojo wake. Tatu, Mkojo
una madhara ya kiafya pia.
Naam, kwa mwanadamu, ni muhimu
kuwa na subra na kutafakari kabla ya kufanya maamuzi. Kwa ndugu zangu
Waislamu, tunaona Mtume Muhammad ameweza kuonyesha hilo.
Na kwa ndugu
zangu Wakristo, kuna mifano pia ya Yesu Kristo kuonyesha subra.
Ndio, Uislamu, kama ilivyo kwa
Ukristo na dini nyingi za humu duniani, msingi wake ni amani na upendo.
Kitendo cha mtoto yule wa Mbagala kukojolea korani kitazamwe kwa sura ya
kitendo kilichofanywa na mtoto .
Na kama ilivyokuwa kwa Bedui
yule, kama pale Mbagala subira na hekima vingetangulizwa, basi, yumkini
tungebaini kuwa mtoto yule hakujua madhara ya kitendo chake. Naye
angekanywa kama tuwakanyavyo watoto wetu. Na hata kitendo hicho
kingefanywa na mtu mzima, bado tulikuwa na haja ya kutanguliza subira na
hekima kumhoji aliyetenda, yaweza akawa kama Bedui yule kwenye msikiti
alimosali Mtume na maswahaba wake.
Na kwa kuangalia picha zile za
Mbagala naiona hatari iliyopo sasa, kuwa tuna vijana wengi wasio na
kazi; Wakristo kwa Waislamu. Vijana wasio na dogo. Ni kama moto
uliofifia. Akipatikana kwa kuchochea kuni wanalipuka.
Ni vijana wanaopatikana wakati
wowote na mahali popote. Hata jambo likianza saa tatu asubuhi wao wapo.
Hawana ofisi wala bosi wa kumwomba ruhusa ya kwenda kuandamana na
kurusha mawe. Ndio hawa wanaonekana wamevaa ‘ Kata kiuno’ na wengi wao
hawajahi hata kuingia misikitini au makanisani.
Inakuawaje kijana wa kweli wa
Kiislamu achome kanisa na kuiba kompyuta. Inakuawaje kijana na muumini
wa kweli wa Kiislamu aonekane saa mchana wa jua kali akivamia baa na
kukimbia na kreti za bia? Ni maswali yanayotutaka tutafakari kwa
makini.
Maana, ninavyoamini mimi, uchumi
na elimu duni ndio hasa vinavyochochea vurugu za kijamii, iwe za kidini
au kisiasa, na hususan inapohusisha vijana. Vijana wetu hawana
misingi mizuri ya elimu, na wengi hawana ajira pia. Haya ni sawa na
makombora yasiyo na gharama kubwa kuweza kutumiwa na wanasiasa wasio
waadilifu na hata viongozi wa kidini wenye mitazamo mikali. Ni
makombora yaliyoanza kutulipukia. Tuliziona ishara, tukazipuuzia.
Leo Kuna vijana watakaotumiwa au
kutumia fursa hiyo kutenda maovu kwa kisingizio cha dini. Ni hawa
wataoshiriki kuchafua taswira za dini husika pia. Tujiadhari, kabla ya
hatari kubwa inayotujia. Hatujachelewa.
Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
http://mjengwablog.com
http://mjengwablog.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)