Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewataka wananchi kuepuka
vurugu zinazohatarisha usalama, na kulinda amani iliyopo nchini
JWTZ imetoa kauli hiyo siku moja baada ya waumini wa dini ya Kiislamu
jijini Dar es Salaam kuandamana sababu ya malalamiko kadhaa kama
kukamatwa kwa Sheikh Issa Ponda na wafuasi wake 49 wiki iliyopita kwa
tuhuma mbalimbali, kutoweka kwa kiongozi wa UAMSHO Sheikh Amir Farid
Hadi, na malalamiko mengine.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, amesema hatua ya wanajeshi
kujitokeza katika kuzima vurugu zilizotokea jijini juzi, ilikua na
lengo la kuwaonyesha wananchi kwamba JWTZ ipo kikazi zaidi, na
anayetaka vurugu atashughulikiwa kisheria.
“Juzi tulionyesha ‘talent show force’ ili watujue kama tupo kazini,
hata kama wametuona tupo kimya, hatuna mzaha katika kulinda na kusimamia
ulinzi na usalama wa taifa hili, kwa hiyo tulikuwa kwenye sehemu ya
utekelezaji wa majukumu yetu, na kwamba atakayekwenda kinyume
tutamshughulikia,” alisema Mgawe.
Alisema zoezi hilo litaendelea kwa maandamano yoyote yatakayoonyesha
dalili za kuhatarisha usalama wa nchi. Aliongeza kwamba wanajeshi
watashiriki kikamilifu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafuata sheria na
taratibu zilizopangwa, bila ya kuathiri usalama wa nchi.
Alisema kwa sasa wanasubiri kibali cha polisi cha kuhusu kuhitaji
msaada ili waweze kuungana nao katika kushughulikia maandamano yenye
lengo la kuhatarisha amani na utulivu.
“Tunawataka wananchi kufuata sheria na taratibu zilizopo na kuepuka
kuhatarisha amani ya nchi, kama wanataka tuingie kazini tutafanya hivyo,
ila tunachowaasa ni kufuata taratibu zilizopo,” alisisitiza.
Katika vurugu za juzi, watu 53 walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki kwenye maandamano.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, watu hao watafikishwa mahakamani Oktoba 22 mwaka huu. Source: Mdimuz blog
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)