Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sila akitoa ufafanuzi
Washiriki wa warsha hiyo wakipiga makofi kwa ishara inayotumiwa na watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi)
Baadhi ya washiriki wa warsha ya siku mbili iliyofadhiliwa na Asasi ya
Kijamii ya The Foundation for Civil Society ilio lenga kutoa mafunzo kwa
maofisa ustawi wa jamii, watendaji kata, kwa kata za Kisiju, Mkuranga
na Kimanzichana kupitia mradi wa ‘Kujenga Uwezo wa Asasi’
Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Wilaya ya Mkuranga,
Khalid Mnyaula (kushoto) ambaye pia ni mratibu wa warsha hiyo
akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sila (kushoto) akifuatilia risala ya
washiriki wa warsha iliyoandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania Wilaya
(CHAVITA), Mkuranga. Wa kwanza kulia ni Mweka Hazina wa
CHAVITA-Mkuranga, Bi. Subira Upuruje ambaye ndiye anayesoma risala hiyo.
Na Joachim Mushi, Mkuranga
CHAMA cha Viziwi Wilaya ya Mkuranga (CHAVITA), kimeiomba
Serikali na wadau wengine kuisaidia jamii hiyo ya walemavu iweze kupata fursa
za elimu kama ilivyo kwa makundi mengine na hatimaye kushiriki kikamilifu
katika shughuli mbalimbali za kijamii ambazo kwa sasa wanazikosa.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini hapa na Mweka Hazina wa
CHAVITA-Mkuranga, Bi. Subira Upuruje alipokuwa akimsomea risala Mkuu wa Wilaya
ya Mkuranga, Mercy Sila katika warsa ya siku mbili kwa maofisa ustawi wa jamii,
watendaji kata, wawakilishi wa vyama vya walemavu na baadhi ya wanachama wa
CHAVITA.
Bi. Upuruje alisema watu wenye ulemavu wa kusikia wilayani
hapo wapo nyuma kielimu, kwani takwimu zinaonesha kati ya viziwi 200 waliopo
eneo hilo ni asilimia 10 tu ndiyo waliopata elimu ya msingi. Alisema hata hivyo
wamekuwawakikosa fursa anuai kutokana na kundi hilo kusahaulika, ikiwemo kukosa
elimu ya kujikinga na Ukimwi, kutoshiriki katika shughuli za kisiasa na huduma
za afya.
“Vituo vya afya vipo hatupati huduma stahili kutokana na
wahudumua kushindwa kuwasiliana nasi…wahudumu wa afya hawajui lugha zetu za
ishara, hatupati taarifa zozote hata zile elimu za masuala ya kujikinga na
Ukimwi. Kwenye siasa tumeshindwa hata kutoa maoni yetu katika mchakato wa Katiba
Mpya hapa kwetu, lugha ya alama kwetu ni tatizo,” alisema Upuruje.
Akijibu risala hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Mercy Sila alisema
kuanzia sasa ofisi yake ipo wazi hivyo kuwataka makundi hayo kupitia kwa
viongozi wao wasisite kumshirikisha katika masuala mbalimbali yanayowatatiza.
“…Sasa mlango u-wazi tushirikiane, nami naahidi kuwapa ushirikiano…nawaagiza
pia watendaji kata, waratibu na maofisa wengine tufanye hivyo,” alisema B.
Sila.
Aliwataka watu wenye ulemavu kutambua kuwa hawajawatenga
katika kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. “Kama inatokea kuna sehemu
inawakwamisha naomba nipewe taarifa mara moja. Kushiriki katika shughuli za
siasa, kijamii na kiuchumi ni haki yenu ya msingi,” alisema Mama Sila.
Aidha alisema sasa umefika wakati wizara ya afya kupeleka
watumishi wao wakasome lugha za alama ili kuweza kuwahudumia makundi mengine ya
walemavu hasa viziwi. Aliwataka wazazi nao kujifunza lugha hiyo ili waweze
kuwahudumia watoto wa aina hiyo kimawasiliano.
Warsha hiyo ya siku mbili iliyofadhiliwa na Asasi ya Kijamii
ya The Foundation for Civil Society imelenga kutoa mafunzo kwa maofisa ustawi wa jamii,
watendaji kata, kwa kata za Kisiju, Mkuranga na Kimanzichana kupitia mradi wa
‘Kujenga Uwezo wa Asasi’.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)