Chama cha Wananchi CUF kinasikitishwa na matukio ambayo hayakutarajiwa
kutokea hapa Zanzibar yaliyoanza kujitokeza tarehe 17/10/2012 ambayo
yamesababisha vurugu kubwa katika Manispaa ya Zanzibar na vitongoji
vyake.
Matukio hayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali za Umma, wananchi mmoja mmoja na hata vyama vya siasa.
Miongoni mwa vitendo hivyo ni ku...
vunjwa Maduka, vyombo vya usafiri, kukatwa miti ovyo na nguzo za umeme,
pamoja na kuchomwa moto maskani za CCM. Matukio mengine ya kusikitisha
na kuhuzunisha kufuatia vurugu hizo ni kuwepo taarifa za kuuwawa kwa
Askari Polisi.
Kutokana na vitendo hivyo, Chama Cha wananchi CUF kinaalaani kwa nguvu
zote matukio hayo ambayo yamepelekea uvunjifu wa mkubwa wa amani ya
nchi, na kusababisha hofu kubwa kwa raia pamoja na wageni wanaotembelea
Zanzibar.
Sambamba na vurugu hizo, Chama Cha Wananchi CUF kimepokea kwa mshtuko
mkubwa taarifa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyotolewa na Waziri
wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Mohammed Aboud Mohammed
iliyoeleza juu ya kutoweka kwa Sheikh Farid Hadi Ahmed katika mazingira
ya kutatanisha.
Katika Taarifa hiyo, Serikali imethibitisha kuwa vyombo vyake vyote vya
ulinzi havijamkamata Sheikh Farid, jambo ambalo limezidisha hofu na wasi
wasi kwa wananchi juu ya mahali alipo na hali yake kiongozi huyo wa
Jumuiya ya Maimamu Zanzibar.
Chama cha Wananchi CUF kinaiomba Serikali kuendeleza juhudi zote za
kuhakikisha taarifa za ukweli na za uhakika zinapatikana juu ya kadhia
ya kutoweka kwa Sheikh huyo kwani Sheikh Farid ni raia wa nchi hii, na
Serikali hii ni kwajili ya wananchi wote, ili kuondoa hofu na wasi wasi
ambao umesababisha baadhi ya wananchi kujengwa na dhana mbaya.
Aidha, Chama cha wananchi CUF kinawataka wanachama wake, wapenzi na
wananchi wote kwa ujumla kutojiingiza na kutofanya vitendo vyovyote
vinavyoweza kupelekea uvunjifu wa amani ya nchi yetu.
Sote kwa pamoja tukatae kabisa kujihusisha na vitendo vya kuleta vurugu
kwa vitendo na kauli zitakazopelekea kuiondolea sifa njema nchi hii ya
Zanzibar ambayo imejijengea duniani kote
Haki sawa kwa Wote
………………………..
Salim Biman
Kaimu Naibu katibu Mkuu Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)