CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kukiburuza Chama cha Mapinduzi (CCM) katika siasa, ambapo kwenye matokeo ya udiwani katika uchaguzi uliofanyika jana, chama hicho kimefanikiwa kutetea kata zake na kunyakua nyingine za CCM. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kukiburuza Chama cha Mapinduzi (CCM) katika siasa, ambapo kwenye matokeo ya udiwani katika uchaguzi uliofanyika jana, chama hicho kimefanikiwa kutetea kata zake na kunyakua nyingine za CCM.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Willbrod Slaa akijumuika kucheza ngoma ya kisukuma iliyokuwa ikitumbuizwa na katika Kijiji cha Lubili, Misungwi, Mwanza. Dkt. Slaa alifika kijijini hapo akiwa katika mizunguko ya mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Lubili. Anayeonekana kushoto akishangilia kwa kupiga makofi ni Mbunge wa Viti Maalum, Leticia Nyerere. Picha na Noise of Silence 
--Hata hivyo uchaguzi huo ambao ulifanyika kwenye kata 29 katika halmashauri mbalimbali nchini, umemalizika huku vurugu kubwa zikitawala na kusababisha wafuasi wa vyama hivyo kuumizana.

Hadi tunakwenda mitamboni matokeo ya kata 14 yalionyesha kuwa CCM ilikuwa imefanikiwa kurejesha kata zake saba, huku CHADEMA ikinyakua kata sita, ambapo mbili zilikuwa za kwao na nne imewanyang’anya CCM na CUF ikiwa na kata moja.

Katika matukio ya vurugu, mbunge wa viti maalumu, mkoani Shinyanga, Rahel Mashishanga (CHADEMA), na katibu wa chama hicho jimbo la Nyang’hwale, mkoani Geita, Michael Ndege, wamenusurika kuuawa baada ya kuvamiwa na kisha kupigwa na kukatwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.

Viongozi hao walifanyiwa unyama huo kwa nyakati tofauti juzi na jana, ambapo Ndege alivamiwa juzi majira ya saa 3 usiku akiwa anaelekea kulala katika nyumba aliyofikia kata ya Lwenzela, saa chache baada ya kumalizika kwa mkutano wa kampeni.

Inadaiwa kwamba akiwa njiani kwenda kulala alivamiwa na kundi la vijana waliokuwa wamevalia sare za CCM, kisha kumkata kwa mapanga na visu, jambo lililosababisha kutokwa damu nyingi na baadaye kukimbizwa hospitali ya wilaya ya Geita.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi usiku kwa njia ya simu, Katibu wa CHADEMA wilaya ya Geita, Rogers Luhega, alisema kwamba kiongozi huyo alivamiwa na kundi hilo kwa mambo aliyodai ni ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Rogers, baada ya tukio hilo waliomba msaada kwa askari polisi waliokuwa wakilinda usalama katani humo, lakini walikataa.

Hata hivyo, alisema usiku wa kuamkia Oktoba 27, mwaka huu, alikoswakoswa kuchomwa mshale na watu aliodai kuwa ni wafuasi wa CCM, ikiwa ni lengo la kudhoofisha nguvu ya chama chake katika uchaguzi huo mdogo kata ya Lwenzela.

Kamanda wa Polisi, mkoa wa Geita, Leonald Paul, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kwa sasa wanafuatilia kwa undani tukio hilo na watu waliohusika ili sheria ifuate mkondo wake.

Kuhusu Mashishanga, inadaiwa kuwa jana majira ya asubuhi alivamiwa na kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM wakati alipokuwa akitembelea kujionea upigaji kura linavyoendelea katika kata ya Mwawaza, jimbo la Shinyanga Mjini.

Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Vincent Nyerere, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na Mashishanga kuvamiwa na kupigwa, gari lake pia lilipondwa kwa mawe na vioo kuharibiwa vibaya.

“Ni kweli nimeambiwa Mashishanga amevamiwa na kupigwa na wafuasi wa CCM wakati akitembelea kuona upigaji kura kata ya Mwawaza. Pia gari yake imepondwa na vioo vinaelezwa vimeharibika vyote,”alisema.

Nyerere aliongeza kuwa mbunge huyo alikuwa na mdogo wake ambaye alipigwa na kuteguka bega la kushoto na kuumizwa sehemu za mdomoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alipoulizwa kuhusuana na taarifa za kuvamiwa na kupigwa kwa mbunge huyo alisema hana taarifa juu ya tukio hilo na aliahidi kufuatilia zaidi.

Katika tukio jingine ambalo Tanzania Daima lilishuhudia, Katibu wa CCM wilaya ya Kahama, ambaye hakufahamika mara moja jina lake, aliingia kwenye kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Bugalama akiwa na sime mkononi.

Katibu huyo aliyekuwa akitumia gari namba T 507 BEW likiwa na nembo ya CCM, inadaiwa alifanya hivyo kwa lengo la kuwatisha mawakala wa CHADEMA waliokuwa wakisimamia kura za mgombea wao, lakini baadaye alitimuliwa.

Mkoani Ruvuma katika kata ya Mletele Manispaa ya Songea, nako wafuasi wa vyama hivyo walichapana kwa mapanga na fimbo na kusababisha zaidi ya watu watano kujeruhiwa wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo.

Tukio hilo ambalo lilitokea juzi saa tisa jioni huko katika kijiji cha Lihumbu, wafuasi wa CHADEMA akiwemo mbunge wao wa viti Maalumu, Chiku Abwao, walivamiwa na kupigwa na wafuasi wa CCM ambao wanadaiwa kuwa walikuwa na gari ndogo.

Hata hivyo wafuasi wa CHADEMA walifanikiwa kulikamata gari dogo la wafuasi wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya hiyo, ambayo ndani yake inadaiwa ilikuwa na mapanga, vipande vya nondo, mundu, fimbo na bundi akiwa hai.

Mmoja wa wafuasi wa CHADEMA Frank Mgao alisema kuwa baada ya kukamatwa gari hilo, askari ambao waliongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, Nico Mwakasanga, waliwakamata na kuwapeleka kituo kikuu cha polisi cha Songea ambako wanaendelea kuhojiwa.

Mgao alisema kuwa baadhi ya wanachama wenzake na wanachama wa CCM wamejeruhiwa kwa kupigwa na panga sehemu mbalimbali za miili yao na wengine wamelazwa katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Ruvuma ambako wanaendelea kupata matibabu zaidi.

Matokeo
Wakati hali ikiwa hivyo, matokeo ya udiwani katika baadhi ya kata yalikuwa yakiendelea kutolewa huku CHADEMA ikiendelea kuiliza CCM kwa kuzitwaa baadhi ya zilizokuwa kata zake.

Jijini Arusha katika Kata ya Daraja Mbili, CCM ilipoteza kata hiyo kwa CHADEMA iliyozoa kura 2192 dhidi ya 1315 za chama tawala.

CHADEMA wameweza kuzirejesha kata zao mbili za Nangerea jimboni Rombo, ambapo mgombea wao Frank Sarakana alijizolea kura 2370 dhidi ya 1134 za Dysmas Silayo wa CCM pamoja na ile ya Mtibwa, mkoani Morogoro.

Wilayani Sikonge katika kata ya Ipole, CCM walipoteza kata hiyo kwa CHADEMA iliyopata kura 577 dhidi ya 372 za washindani wao, na vilevile kuitwaa kata nyingine ya Lengali wilayani Ludewa iliyokuwa ya CCM.

CHADEMA pia ilikuwa ikiongoza katika kata ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, hadi tunakwenda mitamboni usiku.

Nayo CCM ilifurukuta kwa kuzirejesha kata zake za Msalato ya mkoani Dodoma, Bang’ata ya Arumeru Magharibi kwa kuwa 1177 dhidi ya 881 za CHADEMA, Mletele ya Songea CCM ilishinda kwa kura 950 na CHADEMA ilipata 295.

Pia CCM iliweza kutetea kata zake za Mwawaza mjini Shinyanga, Lwenzela mkoani Geita, Bungala wialayni Kahama na Bagamoyo mkoani Pwani kwa kuibwaga CHADEMA wakati Chama cha Wananchi (CUF) kilishinda kata ya Newala.

Nyimbo atimka CHADEMA
Aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA katika jimbo la Njombe Magharibi mwaka 2010, Thomas Nyimbo, jana alitangaza kukihama chama hicho.

Nyimbo ambaye amewahi kuwa mbunge wa CCM kwa miaka 10 katika jimbo hilo kabla ya kutimkia CHADEMA mwaka 2010, alisema hivi sasa atabaki kuwa mwanasiasa huru asiyefungamana na vyama.
Mbele ya mkewe, Mary Mwenga, alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona siasa za kushabikia vyama hazina tija kwa Watanzania walio wengi na badala yake zinawanufaisha viongozi wachache.

Nyimbo alifafanua zaidi akisema kuwa alichojiuzulu ni siasa za vyama, lakini si siasa moja kwa moja, huku akitamba kuwa yeye alizaliwa akiwa ni mwanasiasa, kiongozi na mtu ambaye mawazo yake yanahitajika.

Katika taarifa hiyo aliyoitoa kwa vyombo vya habari mithiri ya mhadhara, Nyimbo alitumia zaidi ya saa moja na nusu kuelezea mustakabali wa taifa na vijana kutokana na vyama vya siasa kuelekea kuwatumbukiza kwenye machafuko.

“Nimeachana na CHADEMA baada ya kubaini kuwa siasa za vyama hazina tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla na ni wakati huu sasa wa kuachana na dhana ya vyama vya siasa vituandalie sera na tunahitaji sasa itungwe sera ya kitaifa ambayo mgombea inabidi atueleze tukimchagua ataitekeleza vipi,” alisema Nyimbo.

Alisema kuwa ikiwa Katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa itakuruhusu mgombea huru, atakuwa tayari kugombea ubunge tena kwenye jimbo lake la Njombe Magharibi, lakini kama Katiba hiyo itazuia fursa hiyo hatogombea tena wadhifa huo maisha yake yote.

Aliongeza kuwa baada ya kupatikana kwa Katiba mpya, inabidi itungwe sera ya taifa itakayolindwa kisheria, ambayo kila chama kitakachofanikiwa kuingia madarakani kilazimike kuifuata badala ya ilivyo sasa vyama vinaogelea hovyo.

Nyimbo alidai kuwa ameamua kujiondoa ndani ya chama hicho baada ya kubaini kuwa kinaenda kinyume na malengo yake kama kinavyojipambanua mbele za watu.

Alisema licha ya kuwaaminisha wananchi, hususan vijana kuwa ndio chama chenye kuleta mabadiliko ya kweli, viongozi wake wa daraja la juu akiwataja Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa wamekuwa wakijinufaisha binafsi.

Kuhusu CCM, Nyimbo alidai kuwa chama hicho kinajimaliza chenyewe kutokana na kuacha suala la rushwa kwenye chaguzi zake za ndani kuwa ndio kigezo muhimu cha kuwapata viongozi wake.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages