Mkuu wa huduma za Elimu ya Makumbusho Zanzibar Ramadhan Machano
akizungumza na Wawakilishi wa vikundi vinavyofanya mazoezi ya viungo
Zanzibar hawapo pichani katika Makumbusho kuu ya Taifa Baitil elajaib
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Washiriki ambao wameenda kuzuru katika maeneo tofauti ya makumbusho ya
Taifa ya Zanzibar wametakiwa kuwa Mabolazi wazuri katika jamii zao ili
kuhakikisha kuwa jamii ya Zanzibar inajenga utamaduni wa kutembelea
katika makumbusho hayo.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa huduma za Elimu ya Makumbusho
Zanzibar Ramadhan Machano katika ziara yake na Wawakilishi wa Vikundi
vitano vinavyofanya mazoezi ya viungo Zanzibar kwa lengo la kuhamasisha
utekelezaji wa mpango wa Utalii kwa wote.
Amesema wameamua kuwaalika wawakilishi hao kutembelea maeneo ya
makumbusho ya Zanzibar ili wasaidie kuwahamsisha wananchi kutembelea
maeneo hayo kwa lengo la kujua historia ya Zanzibar.
Machano amefahamisha kuwa,kwa vile wawakilishi hao wanajumuika na jamii
kwa ujumla anaamini kuwa wanaweza kuibadili jamii na kuepukana na dhana
iliyojengeka kwa wananchi wengi kuwa utalii unafanywa na Wageni.
Aidha amefahamisha kuwa kufanikiwa kwa Mpango wa Utalii kwa Wote
kutaiwezesha Idara ya Makumbusho kutokutegemea wageni katika kupata
mapato yake badala yake Wenyeji wanaweza kuchukua jukumu hilo.
Machano ametaja kingilio ambacho wenyeji wanapaswa kuchangia wanapofika
katika maeneo ya Makumbusho kuwa ni Shilingi 1,000 kwa mtu mzima na
mtoto Shilingi mia tano.
Aidha Machano amesema wataendelea kuwashirikisha viongozi wengine
ikiwemo Mashekh na Walimu wa Shule ili waweze kuisaidia Serikali katika
kuhimiza utalii kwa wote.
Kwa upande wao washiriki wa ziara hiyo wamemuahidi Mkuu huyo kuwa
Wataendelea kuwahamasisha wanachama wao na jamii kwa ujumla ili waweze
kutenga muda wao kwa lengo la kutembelea maeneo ya makumbusho.
Wamesema wamejifunza mengi katika ziara hiyo ikiwemo kujua asili ya
utamaduni wa Mswahili sambamba na kujionea uhalisia wa mambo kinyume na
kusimuliwa katika vitabu vya kihistoria.
Ziara hiyo ambayo ilijumuisha vikundi vya Kata Presha, New Generation,
Obama, Nameless na Mandela ilianzia katika Makumbusho kuu ya Taifa
Baitil Ajaib na kuendelea katika Magofu ya Mwinyimkuu Dunga, Bi
Kihole-Bungi na kumalizia katika Pango la Kuumbi-Jambiani.
IMETOLEWA NA
IDARA YA HABARI MAELEZO
ZANZIBAR 01/09/2012





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)