Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
akibadilishana mawazo na balozi wa Cape Verde nchini Marekani bibi
Fatima Veiga (kushoto). Wa pili kushoto ni balozi wa Tanzania nchini
Marekani bibi Mwanaidi Maajar na kulia ni afisa ubalozi wa Tanzania
nchini humo Suleiman Saleh.
Balozi wa Msumbiji nchini Marekani (kushoto) akibadilishana mawazo na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko
Marekani. Kulia ni balozi wa Cape Verde bibi Fatima Veiga.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
akisalimia na mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Syracuse cha mjini New York Dr.
Horace Campbell. Dr. Horace aliwahi kuwa mkufunzi wa siku nyingi katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa
katika picha ya pamoja na Mabalozi kutoka nchi mbali mbali duniani
wanaoziwakilisha nchi zao nchini Marekani. Mabalozi hao kutoka kushoto
ni balozi Harold Foresyth (Peru), Balozi Mauro Vieira (Brazil) na Balozi
Jorge Arguello (Argentina).
Balozi Jorge Hernandez wa Honduras (katikati), akisisitiza jambo wakati
akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad huko nchini Marekani. Kulia ni Balozi wa Brazil nchini Marekani,
Mauro Vieira.Picha zote na mpiga picha maalum, New York
----
Na Mwandishi Maalum, Marekani
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekutana na mabalozi wa nchi mbali mbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Marekani na kubadilishana mawazo juu ya masuala tofauti yakiwemo ya kiuchumi, afya na teknolojia ya habari.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekutana na mabalozi wa nchi mbali mbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Marekani na kubadilishana mawazo juu ya masuala tofauti yakiwemo ya kiuchumi, afya na teknolojia ya habari.
Katika mazungumzo yake na balozi wa Malaysia nchini Marekani bwana
Othman Hashim, Maalim Seif amesema Zanzibar inaweza kushirikiana na
Malaysia katika maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu ya
juu, biashara, uwekezaji na kilimo.
Maeneo mengine ambayo Zanzibar na Malaysia zinaweza kushirikiana ni
teknolojia ya habari, benki za kiislamu na utalii.
Katika mazungumzo hayo viongozi hao pia wamekubaliana juu ya suala la
kufuatilia mazungumzo hayo ambapo Zanzibar itatuma maofisa wake nchini
Malaysia, ili kuona namna ya kukuza mahusiano yaliyopo baina ya nchi
hizo mbili.
Kabla ya kukutana na mabalozi hao, Makamu wa Kwanza wa Rais alipata
fursa ya kushiriki kwenye mikutano na makongamano mbali mbali juu ya
mambo ya siasa na mahusiano ya kimataifa yaliyoandaliwa na taasisi ya
National Democratic Institute mjini North Carolina, Marekani.
Makamu wa Kwanza wa Rais pia amefanya mazungumzo na mkuu wa taasisi
inayojishughulisha na utoaji wa misaada ya vifaa vya hospitali katika
nchi mbali mbali duniani Bwana Abdul Makembe Kimario.
Katika mazungumzo yao viongozi hao walijadiliana juu ya uwezekano wa
Zanzibar kuweza kufaidika na misaada hiyo ya vifaa vikiwemo vitanda vya
kulazia wagonjwa, vitanda maalum vya kufanyia upasuaji na mashine za
uchunguzi wa maradhi mbali mbali katika hospitali zake za Wilaya na
hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Taasisi hiyo imekuwa ikijishughulisha na utoaji wa misaada ya vifaa vya
hospitali kwa zaidi ya nchi 124 duniani zikiwemo China, India na
Israel.
Maalim Seif pamoja na viongozi na mabalozi wa nchi mbali mbali pia
walihudhuria katika kongamano maalum, ambapo walishuhudia viongozi wa
vyama vya Republican na Democratic vya nchini Marekani wakihojiwa na
waandishi wa habari kuhusiana na kampeni za uchaguzi unaotarajiwa
kufanyika Novemba 6 mwaka huu nchini humo, ambapo chama cha Demcratic
kinawakilishwa na Rais wa sasa wa Marekani Rais Barack Obama na chama
cha Republican kinawakilishwa na Bwana Mitt Romney.
Makamu wa Kwanza wa Rais aliwasili nchini Marekani tarehe 02 mwezi huu kwa ziara ya kikazi.
Katika uwanja wa ndege wa New York alipokelewa na Balozi wa kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvaku Manongi na huko Mjini
North Carolina alipokewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani bibi
Mwanaidi Sinare Maajar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)