Rais Jakaya Kikwete akipeana Mkono na Naibu Waziri Mkuu wa China, Hui Liangyu alipomtembelea ikulu, Dar es Salaam.

Rais Jakaya Kikwete akimkaribisha ikulu Jijini Dar es Salaam jana Naibu Waziri Mkuu wa China, Hui Liangyu
--

Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
jana, Jumatano, Septemba 5, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Hui Liangya
kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika
mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam mara tu baada ya
Mheshimiwa Liangya kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu katika
Tanzania kama sehemu ya ziara ya nchi za Afrika, viongozi wote wawili wameeleza kuridhishwa kwao na hali na ustawi wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais
Kikwete ametumia nafasi ya ziara hiyo ya Mheshimiwa Liangya kuishukuru
China kwa michango yake katika jitihada za maendeleo za Tanzania.
Amesema Rais Kikwete: ”Jamhuri
ya Watu wa China imetusaidia mengi katika jitihada zetu za maendeleo
kuanzia kwenye ujenzi wa Reli ya TAZARA, ujenzi wa Uwanja wa Taifa,
ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, ujenzi wa
bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam, ujenzi wa Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano, na ahadi ya kusaidia kuanzisha Benki ya Kilimo
Tanzania. Kwa hakika Jamhuri ya Watu wa China imetusaidia mengi na
tunaishukuru sana.”
Rais Kikwete pia ameitaka China kuendelea kuisaidia Tanzania hasa katika maeneo ya jinsi ya kuongeza kasi ya uchumi. “Tunataka
kwa kweli kujifunza kutoka mifano ya mafanikio ya marafiki zetu wa
karibu kama China. Hivyo, bado tunaendelea kusisitiza ushirikiano wa
China katika kuanzisha na kuendesha maeneo maalum ya uzalishaji –Special
Economic Zones “
Naye
Mheshimiwa Liangya amemwambia Rais Kikwete kuwa China itaendelea
kuimarisha uhusiano wake na Tanzania ambao umekuwa unashamiri tokea
ulipoanzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao
Tse Dung.
Mheshimiwa
Liangya amesema kuwa undani wa miradi yote ambayo China inasaidia
katika Tanzania ungejadiliwa kwenye mkutano kati yake na Waziri Mkuu
Mheshimiwa Mizengo Pinda katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika baada
mchana wa jana
Kiongozi
huyo wa China pia ameisifu Serikali ya Mheshimiwa Kikwete kwa uamuzi
wake wa kuanzisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na kuongeza kuwa
mpango huo umeandaliwa kwa umakini mkubwa. “Nawapongezeni
kwa uamuzi wenu wa busara wa kuanzisha tena Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano. Ukitekelezwa vizuri unaweza kusukuma kwa kasi zaidi
maendeleo ya nchi yetu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
5 Septemba, 2012





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)