Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
akisalimiana na viongozi wa Jumuiya ya tiba asilia Zanzibar JUTIJAZA,
waliokutana ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kubadilishana mawazo
juu ya maendeleo ya tiba hiyo nchini.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na
Mkurugenzi wa mambo ya nje ofisi ya Zanzibar, balozi Silima Kombo Haji
ofisini kwake Migombani Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisikiliza kwa umakini maelezo yanayotolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Tiba Asilia Zanzibar JUTIJAZA,
Dkt. Haji Juma Msanifu kuhusiana na maendeleo ya tiba hiyo Zanzibar,
huko ofisini kwake Migombani Zanzibar.Picha, Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar
--
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim
Seif Sharif Hamad amesema mabalozi pamoja na idara ya mambo ya nje
Zanzibar, wanayo nafasi kubwa ya kuisaidia Serikali kukuza mahusiano
yake na nchi nyengine pamoja na mashirika ya kimataifa.
Amesema
licha ya suala la mambo ya nje kuwa la Muungano, lakini yapo baadhi ya
mambo ambayo Zanzibar inaweza kuyafanya katika kushirikiana na mataifa
mengine, kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Maalim
Seif ametoa changamoto hiyo ofisini kwake Migombani Zanzibar, alipokuwa
na mazungumzo na Mkurugenzi wa mambo ya nje ofisi ya Zanzibar, balozi
Silima Kombo Haji.
Amefahamisha kuwa Zanzibar kama nchi imekuwa ikitembelewa na viongozi mbali mbali wa nchi za
kigeni pamoja na mashirika ya kimataifa ambao wamekuwa na hamu na
shauku ya kutaka kuendeleza mahusiano na Zanzibar, katika nyanja tofauti
zikiwemo za kiuchumi.
“Wakuu wa nchi mbali mbali wanakuja hapa Zanzibar pamoja na viongozi wa mashirika ya kimataifa, na huwa na shauku kubwa na kutaka kuendelea mahusiano baina yao na nchi yetu”,alieleza.
Amempongeza
mkurugenzi huyo kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo, na kwamba serikali
itampa mashirikiano ya kutosha katika kutekeleza majukumu yake, na
kusifu kazi nzuri inayofanywa na ofisi hiyo.
Hata
hivyo Makamu wa Kwanza wa Rais amemtaka mkurugenzi huyo na ofisi yake
kwa ujumla, kuongeza umakini wakati wanaposhughulikia safari za viongozi
wakuu wa nchi, ili kuondosha usumbufu unaoweza kujitokeza.
Kwa
upande wake balozi Silima ambaye alikwenda kujitambulisha kufuatia
uteuzi wake wa hivi karibuni, amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais
kuwa ofisi yake itafanya kazi kwa karibu na serikali katika kuhakikisha
kuwa Zanzibar inapata fursa zinazostahiki.
Wakati
huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais amekutana na uongozi wa Jumuiya ya
tiba asilia Zanzibar JUTIJAZA, na kubadilishana mawazo juu ya maendeleo
ya tiba hiyo nchini.
Katibu
Mkuu wa Jumuiya hiyo Dkt. Haji Juma Msanifu amesema jumuiya yake ina
mpango wa kuanzisha vitalu maalum vya miti asilia, ili kurahisisha
upatikanaji wa dawa hizo.
Dkt.
Msanifu amesema wamefikia uamuzi huo kufuatia kuendelea kwa vitendo vya
ukataji wa miti ovyo, hali inayotishia kutoweka kwa miti inayotumika
kwa ajili ya upatikanaji wa dawa asilia.
Nae
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo bi Zahra Hassan amesema jumuiya yao
bado inakabiliwa na tatizo la ofisi za uhakika pamoja na usafiri, na
kuiomba serikali kuangalia namna ya kuisaidia ili kuondokana na matatizo
hayo.
Amesema
tiba asilia ni muhimu na zimekuwa zikitumika kitaalamu na kujipatia
umaarufu mkubwa katika nchi za Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla,
jambo ambalo linapaswa kupewa msukumo kwa maslahi ya wananchi na taifa
kwa ujumla.
Maalim
Seif kwa upande wake amewataka wanajumuiya hao kufuatilia upatikanaji
wa hati miliki za viwanja walivyonavyo kwa ajili ujenzi wa ofisi na
kituo cha utafiti, ili waweze kufanikisha matarajio yao kwa uhakika.
Kuhusu
ukataji wa miti, Maalim Seif amesema bado ni changamoto inayoikabili
ofisi yake, lakini wanaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa
wananchi wanapata elimu ya kutosha juu ya uhifadhi wa miti na mazingira
kwa ujumla.
Na
Hasssan Hamad
Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)