NA MWANDISHI WETU, MWANZA
L Yataka usichukue muda mrefu
L Yataka ubaini pia mazingira ya kuuawa mwandishi huyo.
L Yatoa pole kwa wafiwa, Wanahabari na Watanzania.
CCM imevitaka vyombo na tume
zilizoundwa kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi,
vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini kila kitu ikiwemo
chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira yaliyosabaisha kipigo
hadi kufa mwandishi huyo.
Aidha imetaka uchunguzi
usichukue muda mrefu ili ukwelikuhusiana na kadhia hiyo ujulikane mapema
na hatua zichukuliwe kwa kila atakayebainika kuwa sababu au chanzo cha
vurugu na kifo cha mwandishi huyo.
Aidha imesema imepokea kwa
masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari
watatu wa Polisi wakati wa vurugu hizo na kimetoa pole kwa wafiwa,
wanahabari wote nchini na wote walioguswa na msiba huo kwa namna moja au
nyingine.
Hayo yamesemwa na Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye katika
taarifa ya CCM kwa vyombo vya habari, leo jijini hapa, kuhusiana na
sakata la vurugu hadi kifo cha mwandishi huyo, juzi mkoani Iringa.
“Itakumbukwa tarehe Septemba 2,
2012 katika operesheni za CHADEMA mkoani Iringa kulitokea vurugu
zilizosababisha kuuawa kwa mwandishi wa habari mzoefu,nDaudi Mwangosi na
kujeruhiwa vibaya kwa polisi watatu wa kikosi cha kutuliza ghasia.
Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa
za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari hao”, Nape alisema katika taarifa
hiyo, na kuongeza:
“CCM inachukua nafasi hii kutoa
pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote walioguswa na msiba huu kwa
namna moja au nyingine na tunatoa mwito kwa vyombo na tume mbalimbali
zilizoundwa kuchunguza swala hili, vichunguze kwa umakini na weledi
mkubwa ili kubaini yote – ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na
mazingira ya kifo cha ndugu yetu”.
Alisema CCM inasikitishwa na
mfululizo wa matukio ya watu kupoteza maisha au kujeruhiwa katika
mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na CHADEMA nchini hasa
zile zilizofanyika kwa kukaidi amri halali za vyombo vya ulinzi na
usalama.
Alikumbusha baadhi ya matukio
hayo kuwa ni pamoja na lile la kuuawa kwa kada wa CCM Mkoani Singida,
kuuawa kwa Ally Hassan mjini Morogoro na la juzi la kuuawa kwa Mwangosi
Mjini Iringa, kujeruhiwa kwa askari polisi Iringa na matukio mengine
mengi ambayo yametokea wakati CHADEMA wakiendesha operesheni zao
mbalimbali nchini.
“Matukio haya si mazuri kutokea
kwenye shughuli za Chama cha siasa. Kwakweli ni aibu, inayohitaji
uwajibikaji,hata kama ni wa kisiasa. Inapotokea shughuli za chama chako
zinasababisha kupotea kwa maisha ya watu kila unapozifanya na bado
usitake kuwajibika, inahitaji roho ngumu na ujasiri wa aina yake”
alisema Nape katika taarifa hiyo na kuongeza;
“Inakuwa mbaya zaidi pale vifo
hivi vinaposababishwa na Chama hicho kutotii amri halali zilizotolewa
kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi inayovipa pia uhalali vyama vya
siasa kuwepo na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria”.
“Laiti Chama hicho kingesubiri
siku chache zilizobakia kabla ya Sensa kuisha kabla ya kuendelea na
mikutano yake ni dhahiri mauaji haya yasingetokea. Lakini kauli za
kukebehi na uamuzi wa kukaidi amri ya Jeshi la Polisi na kusema “tupo
tayari kwa lolote” ni ishara kwamba Chama hiki kiliandaa na kujiandaa na
fujo zilizotokea”, alisema Nape.
CCM imetoa mwito kwa vyama vya
siasa na wanasiasa kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa
sheria na kusema kwamba amani na utulivu vilivyopo nchini ni kazi nzuri
iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa la Tanzania kwa kujenga
utamaduni wa kuzingatia utawala wa sheria.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)