CCM UINGEREZA NAO WAFUNGUA SHINA JIPYA LA LEICESTER KWA HOJA NA KISHINDO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

CCM UINGEREZA NAO WAFUNGUA SHINA JIPYA LA LEICESTER KWA HOJA NA KISHINDO



Picha mbalimbali za wanachama wapya wa CCM wakichukua kadi zao muda mfupi baada ya uzinduzi wa shina Jipya katika Mji wa Leicester 
---
Chama Cha Mapinduzi ,Tawi la  Uingereza Jana Tarehe 09.09.12 kimefungua shina Jipya katika Mji wa Leicester kwa changamoto ya hali ya juu, hoja nzito na kishindo kikubwa.
Katika ufunguzi huo uliosimamiwa na Katibu Mpya wa Tawi Bi. Mariam Mungula alisisitiza suala la umoja kwa wana CCM na wanadiaspora kwa ujumla katika kutoa mchango wao kwa sauti moja ili kuweza kuwa na Nguvu ya pamoja na kuchangia katika  kuboresha ufanisi wa Serikali ya Tanzania kwenye Nyanja mbali mbali za huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi kwa faida ya watanzania wote. 

Awali Bi. Mungula alitoa salamu kutoka kwa Mh. January Makamba kama Katibu wa NEC Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa ambae aliwahakikishia wana CCM Diaspora kuwa , CCM huko nyumbani ,akiwemo Mwenyekiti wa Taifa ,Mheshimiwa Jakaya Kikwete inathamini sana imani ya wanachama wa Diaspora na kazi wanayofanya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi. Mh. January Makamba aliahidi wana Diaspora kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaweka mfumo mzuri ili kuyatumia mawazo ya wana CCM walioko nje ya Nchi ili  kukiimarisha Chama.

Viongozi wa Shina Jipya la CCM Leicester waliochaguliwa ni kama wafuatavyo:
  1. Cletus Shigela – Mwenyekiti
  2. Moses Kusamba – Katibu
  3. Hussein Hussein – Mjumbe
  4. Pauline Nzengula – Mjumbe
  5. Agness J Nyehunge - Mjumbe
    6. Mzee Khalid Kassim Ndagiye (Mlezi)
Katika ufunguzi huo ambao ulihudhuliwa na wana Leicester wengi , hoja mbalimbali katika masuala ya kukiendeleza chama katika utawala wa nchi zilijadiliwa na kutolewa ufafanuzi na viongozi wa Tawi akiwemo Mh. Haruna Mbeyu “Special Advisor”, Bw. John Lyimo - Uchumi na Fedha, Bw. Abraham Sangiwa Naibu Katibu Uenezi na Siasa Tawi na Bw. Albert Ntemi Naibu Katibu Tawi.

Baada ya mahojiano na Uongozi wa Tawi  na kujibu maswali yaliyokuwa yakiwasumbua wanachama, wakereketwa na makada wengi , wanachama wapya wengi walijitokeza na kujiunga na CCM papohapo na kukabidhiwa Kadi za uanachama na Katibu wa Tawi Bi. Mungula,huku wakishangiliwa na kupongezwa na wanachama wenzao na uongozi mpya wa Tawi la CCM UK. Waliobaki katika wahudhuriaji hao walishakuwa na kadi za Chama Cha Mapinduzi zamani na hivyo walionyesha furaha kubwa kuwa sasa wataweza kuzitumia kadi zao baada ya kuwa na Shina katika mji wao.

Kabla ya uchaguzi wa viongozi wa shina jipya ambao uliendeshwa kwa demokrasia ya hali ya juu,  akijibu hoja za wana Leicester Naibu Katibu wa Siasa na Uenezi wa Tawi Bw. Abraham Sangiwa aliwakumbusha wajumbe kuzifahamu haki, sifa na wajibu wa uanachama na miiko ya uongozi kama ilivyoainishwa katika miongozo na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.
     Kidumu Chama Cha Mapinduzi

Mariam Mungula
Katibu wa Tawi la Chama Cha Mapinduzi, Uingereza
                        CHAMA CHA MAPINDUZI -UK.                     
Imetolewa na Idara ya Siasa na Uenezi, Tawi la CCM ,Uingereza.
Tarehe: 10 Septemba 2012.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages