Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kuwepo
ugonjwa wa Ebola ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo
yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Kanda ya Magharibi ya nchi hiyo ambapo takriban watu
20 wamepata maambukizo na kati yao, 14 wamepoteza maisha. Hadi kufikia tarehe
29 Julai 2012 kuna wagonjwa wawili waliolazwa na hali zao zinazidi kuimarika.
Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote
katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo
inapakana na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma na
Rukwa).
Chanzo na dalili za ugonjwa wa Ebola
Ugonjwa wa Ebola
husababishwa na virusi vya Ebola. Dalili zake ni homa kali ya ghafla, kulegea
mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa, na vidonda kooni. Mara nyingi dalili
hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa
kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa damu ndani na nje mwilini.
Kipindi cha
kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 21 baada ya kupata maambukizi.
Kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola
Ugonjwa wa Ebola
unaambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa njia zifuatazo:
o Kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo
o Kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huu.
o Kugusa wanyama walioambukizwa (mizoga na wanyama wazima) kama vile sokwe na
swala wa msitu.
Tiba na chanjo ya Ebola
Mpaka sasa ugonjwa wa
Ebola hauna tiba wala chanjo.
Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la
ugonjwa huu nchini:
o
Kutoa taarifa ya
tahadhari kuhusu ugonjwa huu kupitia kwa waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya.
Aidha, taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa
(Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa,
Mwongozo kwa watumishi wa sekta ya afya wa namna ya kuchukua sampuli na
vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.
o
Kuimarisha ufuatiliaji
wa ugonjwa huu kupitia kwa wataalam wa Afya katika Mikoa, Wilaya na Maeneo ya
mipaka. Aidha, watalaam wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za
ugonjwa huu, ili endapo ugonjwa huo ukitokea uweze kutolewa taarifa mapema.
o
Kupeleka vifaa kinga kwa
ajili ya watumishi wa afya.
Wito
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyeripotiwa hapa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha
kutolea huduma za afya kilicho karibu, mara watakapoona mgonjwa yeyote
atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Regina
L. Kikuli
KAIMU
KATIBU MKUU
31/7/2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)