Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania
akisalimiana na Rais Joyce Banda wa Malawi wakati walipokutana kwenye
mkutanoa wa SADC nchini Msumbiji hivi karibuni
Na. Aron Msigwa – MAELEZO. Lilongwe, MALAWI.
Tanzania imeitaka Malawi kusitisha
shughuli za utafiti katika eneo la ziwa Nyasa lenye mgogoro na
kusisitiza nia yake ya kuendelea kuzungumza na nchi hiyo kuhusu mgogoro
wa mpaka licha ya nchi hiyo kuendelea na msimamo wake wa kumiliki eneo
lote la ziwa hilo.
Hayo yamebainishwa katika mkutano
wa wataalam na viongozi kutoka serikali ya Malawi na Tanzania kushindwa
kufikia muafaka uliokusudiwa kuhusu eneo halali la mpaka unaotenganisha
nchi hizo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha
kikao cha usuluhishi kilichohusisha timu za wataalam na viongozi wa
wizara husika wa nchi hizo kilichomalizika jana usiku mjini Lilongwe
Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Bernard
Membe amesema Tanzania bado inaamini katika mazungumzo ili kufikia
muafaka wa kudumu wa mgogoro huo.
Amesema kuwa pamoja na sababu
mbalimbali zilizotolewa na upande wa serikali ya Malawi juu ya umiliki
wa eneo lote la ziwa Nyasa ,msimamo wa Tanzania juu ya mpaka
unaozitenganisha nchi hizo uko wazi kwa kwa kuzingatia vielelezo vya
historia vilivyoachwa na wakoloni na sheria za kimataifa kuhusu mpaka
kuwa katikati ya ziwa hilo.
Ameeleza kuwa licha ya serikali ya Malawi kuonyesha kila dalili za kukwamisha mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao mbalimbali nchini humo viongozi wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu uliomalizika jana usiku wameamua kuunda timu za wataalam
Ameeleza kuwa licha ya serikali ya Malawi kuonyesha kila dalili za kukwamisha mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao mbalimbali nchini humo viongozi wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu uliomalizika jana usiku wameamua kuunda timu za wataalam
“Licha ya kuwasilisha vielelezo
kuonyesha uhalali wa mpaka hatukuweza kufikia muafaka tumefika mahali pa
kuhitaji msaada tuzitume tume za nchi zetu zitoe mapendekezo ya nini
kifanyike maana kuna kila dalili kwamba sisi wenyewe tutashindwa
kuendelea zaidi “
Amesema kuwa wataalam kutoka
Malawi na Tanzana watakutana mwezi Septemba jijini Dar es salaam ili
waweze kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuwapata wasuluhishi wa
mgogoro huo pamoja na kutoa mapendekezo ya faida na hasara ya njia
watakazozipendekeza.
“ Sasa tumefika mahala pa kuhitaji
msaada,tutazituma timu zetu zikae pamoja na kutoa mapendekezo ya nini
kifanyike maana inaonyesha wazi kabisa sisi wenyewe hatutaweza kuendelea
tena sasa timu zitatoa mapendekezo juu ya kesi hii tuwaite wazee wenye
busara barani Afrika tunaowaamini watuamulie” amesema.
Amefafanua kuwa timu za wataalamu
zitakazoundwa zinatarajia kukutana mwezi Septemba jijini Dar es salaam
ili kutoa mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa marais wa nchi hizo katika
kuelekea hatua ya pili ya utatuzi wa mgogoro huo ikiwemo kumtafuta
msuluhishi au kwenda kwenye mahakama ya Kimataifa.
Aidha , Tanzania imeitaka Malawi
kusitisha shughuli za utafiti katika eneo la Tanzania katika ziwa Nyasa
lililo na mgogoro na kukisisitiza kuwa mchakato wote wa kutafuta suluhu
utaendeshwa kwa amani na utulivu huku akiwaomba watanzania kuendelea
kuiombea nchi amani ili suala hilo limalizike kwa amani ,utulivu na
undugu.
Kwa upande wake waziri wa Mambo ya
Nje na Mahusiano ya kimataifa wa Malawi Bw. Ephraimu Chiume katika
maelezo yake wakati wa kuhitimisha mkutano huo amesisitiza kuwa licha ya
mgogoro huo kuhitaji busara zaidi bado serikali yake inaamini kuwa
mpaka kati yake na Tanzania uko upande wa mashariki mwa ziwa Nyasa na
unatenganishwa na ardhi ya Tanzania.
Amesema kutokana na unyeti wa
suala lenyewe na eneo hilo pamoja na historia ya nchi yake anapenda
kuona ufumbuzi ukipatikana haraka ili wananchi wa nchi mbili waweze kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
“Ni matumaini yangu mkutano wa Dar
es salaam utaofanyika mwezi Septemba utazaa matunda ili suala hili
lipatiwe ufumbuzi na ikiwezekana tupate msaada wa sheria za kimataifa
kwa sababu suala hili liko kisheria zaidi” alisisitiza Bw. Chiume.
Ujumbe wa wataalam kutoka Tanzania
uliokuwa ukitafuta suluhu ya mgogoro huo uliwahusisha makatibu wakuu
Patrick Lutabanzibwa (Ardhi),John Haule(Mambo ya nje) na mawaziri wa
wizara ya Ardhi Prof. Anna Tibaijuka na Bernard Membe wa Mambo ya Nje
na ushirikiano wa Kimataifa, balozi wa Tanzania nchini Malawi Patrick
Tsere pamoja na wataalam wanaotoka eneo la ziwa Nyasa akiwemo
Prof.Hemphrey Kamisama ambao nao walitoa maelezo kueleza hisia za
wananchi wa eneo hilo na uhalisia wa ziwa hilo
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)