TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUWEPO KWA MGONJWA WA EBOLA, WILAYA YA KARAGWE MKOA WA KAGERA, TANZANIA
Utangulizi
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu
tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbali mbali
vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani Karagwe mkoa wa
Kagera.
Mnamo
tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na Ustawi Wa Jamii ilipokea
taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya kuwepo kwa
mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola, katika
hospitali ya Wilaya ya Nyakahanga.
Aidha,taarifa
hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye
umri wa miaka (6|) kutoka katika kijiji cha Nyakatundu wilayani
Karagwe. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali, kulegea, kutokwa
damu puani, kutapika damu, na kukojoa damu.
Maelezo
kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu alianza kuugua kuanzia
tarehe 30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin baada ya
hospitali binafsi kuonyesha kuwa ana ugonjwa wa“Typhoid”.
Uchunguzi
wa awali katika hospitali ya Nyakahanga ulionyesha kuwa mtoto huyu
alikuwa anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja ndogo (Urinary Tract
Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na Vipimo vya
malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo kwa magonjwa haya.
Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa
na mama yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili
ya uangalizi zaidi.
Aidha
mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za wataalamu kutoka Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Kagera imeweza
kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua sampuli za damu
kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya uchunguzi wa
magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika na
ugonjwa wa Ebola.
Timu
hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa huyu kwa sasa
imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa damu
kumekoma pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa
hana dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu
mwingine yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au
cha jirani kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;
• Imepeleka
timu ya wataalamu mbali mbali kutoka Wizarani na mkoa kwa lengo la
kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo.
• Imetoa
elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea ugonjwa wa Ebola pamoja na
dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi wa afya katika
hospitali ya Nyakahanga
• Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
• Kutoa
matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza sauti na kupitia radioni
(Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu. Aidha, vipeperushi pia vimetolewa.
Hitimisho
Wizara
inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa nchini.Aidha, Wizara ya
Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu iwapo utatokea
hapa nchini.
Kwa
sasa timu za wataalum zipo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera,
Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa
wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa huu sehemu za
mipakani.
Wizara
inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa haraka kwenye kituo
chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona dalili za ugonjwa
huu.
Imetolewa na:
kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 6 Agosti, 2012.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)