Naibu waziri wa Maliasili na Utalii
Mh.Lazaro Nyalandu akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Meatu
alipotembelea pori la akiba la Maswa.Nyuma yake ni mbunge wa jimbo la
Kisesa mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa wilaya ya Meatu, Rosemary
Kirigini akitoa taarifa yake ya maendeleo ya pori la akiba Maswa kwa
naibu Waziri Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu aliyetembelea pori
hilo.
Mbunge wa jimbo la Kisesa wilaya ya Meatu Mh. Mpina akitoa salamu zake kwa wafanyakazi na viongozi wa pori la akiba Maswa.
Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu akizungumza na wafanyakazi na viongozi wa pori la akiba Maswa.
Naibu Waziri wa Maliasli na Utalii
Mh.Lazaro Nyalandu (kushoto) akibadilishana mawazo na mbunge wa jimbo la
Kisesa mkoa wa Simiyu Mh. Mpina muda mfupi baada ya kuwasili uwanja wa
ndege wa pori la akiba la Maswa.
Baadhi ya viongozi waliofuatana na
naibu waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu kwenye boti kwenda
kukagua maendeleo ya hifadhi ya kisiwa cha Saanane.
Naibu waziri wa Maliasili na Utalii
Mh.Lazaro Nyalandu (kulia) akiwa kwenye boti akielekea kukagua hifadhi
ya kisiwa cha Saanane jijini Mwanza. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na.NATHANIEL LIMU
Serikali imeahidi kutoa kiasi cha 6M/-
kulipa fidia ya ng’ombe 22 wanaodaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na
askari wa wanyamapori wa pori la akiba Maswa wilayani Meatu, mkoani
Simiyu.
Inadaiwa ng,ombe hao walipigwa risasi na
kuuawa Desemba 2009 baada ya kuingizwa kuchungia ndani ya hifadhi hiyo,
kitendo ambacho ni kinyume na sheria zinazolinda hifadhi za wanyama pori
.
Ahadi hiyo imetolewa juzi na Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akizungumza kwenye
mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wakazi wa kata ya Sakasaka jimbo la
Kisesa.
Alisema lengo la uamuzi huo ni kuimarisha
mahusiano mazuri kati ya askari wa wanayamapori na wakazi wa vijiji
vinavyozunguka akiba ya pori hilo.
“Pia ni sehemu ya mikakati inayochukuliwa
na serikali ya kuhakikisha mgogoro wa muda mrefu kati ya uongozi wa
pori la akiba Maswa na wananchi wakazi wa vijiji vinavyozunguka pori
hilo,unamalizika na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo,”
alisema Nyalandu.
Katika hatua nyingine, Nyalandu ambaye
pia ni mbunge wa jimbo la Singida kaskazini, alisema kuwa serikali
inatarajia kuunda kamati huru ambayo itashughulikia kutafuta ufumbuzi wa
mgogoro uliopo kwa muda mrefu katika akiba ya pori la Maswa.
“Katika kamati hii,kutakuwepo na
mwakilishi mmoja kutoka wizara ya mali asili na utalii na wajumbe
watakaobaki watakuwa ni watu huru ambao watazitendea haki pande zote
mbili. Ni matarajio yetu kwamba taarifa itakayotolewa na kamati hiyo
haitaionea au kupendelea upande wo wote, itakuwa timilifu,” alifafanua
naibu waziri huyo.
Nyalandu alisema kamati hiyo itatoa taarifa yake wizarani mapema kabla bunge la sasa kuhairishwa.
Katika hatua nyingine, alitumia fursa
hiyo kuagiza wananchi waendelee kuelimishwa vya kutosha juu ya sheria
zote za hifadhi za wanyama pori ili waweze kuzitii bila ya
kushurutishwa.
“Napenda kukumbusha kuwa marufuku
kuchungia,kulima,kuingiza au kufanya shughuli zo zote za kijamii ndani
ya hifadhi la wanyama pori. Mfugaji au mtu yeyote atakayevunja sheria
halali ailizowekwa atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema
Nyalandu.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini, alisema hifadhi ya pori la akiba Maswa ipo kwa mujibu wa sheria.
“Kwa hiyo, wananchi kuigiza mifugo yao
ndani ya hifadhi hiyo kwa madai ya kutokuwa na maeneo ya malisho ni
kuvunja sheria.
Tunashauri wananchi wenye mifugo wanaopakana na pori la
akiba la Maswa watafute maeneo mengine ya kupeleka makundi yao ya
mifugo, au washauriwe kupunguza mifugo yao kwa kuanzisha ufugaji wa
kisasa,” alisema DC Kirigini.
Aidha, alisema kuwa wataendelea kutoa
elimu ya uhifadhi kwa madai kwamba hifadhi zilizopo, ni hazina kwa
vizazi vilivyopo sasa na vya baadaye kwa nchi ya Tanzania na dunia kwa
ujumla.
Wakati huo huo, DC Kirigini ameiomba
serikali kuangalia uwezekano wa kubadilisha jina la akiba la pori la
Maswa na kulipa jina la akiba ya pori la Meatu.
Alisema kuwa kwa vile sasa wilaya ya
Maswa imegawanywa na kuwa na wilaya wilaya tatu baada ya kuanzishwa kwa
wilaya ya Bariadi na Meatu,akiba ya pori hilo ambalo sehemu kubwa ipo
wilaya mpya ya Meatu,hivyo kuna ulazima wa kuitwa pori la akiba la
Meatu.
Kwa upande wake Nyalandu alisema ombi hilo la kubadilisha jina la pori hilo linazungumzika.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)