Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak
akisalimiana na wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani
waliofika ofisini kwake Migombani. Kutoka kushoto ni Bw. Douglas Bruce
na Barrot Lambdin.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak
akizungumza na wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani waliofika
ofisini kwake Migombani
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak
akizungumza na wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani waliofika
ofisini kwake Migombani. Kutoka kushoto ni Bw. Douglas Bruce na Barrot
Lambdin.
Mkurugenzi wa Tume ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar
Bwana Ahmed Salim Awadh akifafanua jambo katika kikao kilichowajumuisha
wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani kilichofanyika ofisini
kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani. Picha na
Salmin Said Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
--
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr. Omar Dadi
Shajak amesema mikakati na misaada zaidi inahitajika katika kupambana
na uingizaji wa dawa za kulevya, sambamba na kupunguza maambukizi ya
virusi vya Ukimwi Zanzibar.
Amesema Zanzibar ambayo ni nchi ya visiwa, itaweza kudhibiti uingizaji
na utumiaji wa dawa kulevya iwapo kutakuwa na mikakati imara na
uungwaji mkono kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi
Dr. Shajak ametoa kauli hiyo Ofisini kwake Migombani alipokuwa na
mazungumzo na wataalamu wa taasisi ya Pangaea ya nchini Marekani
inayojishughulisha na utoaji wa huduma mbali mbali za kiafya zikiwemo za
ushauri na tiba kwa watumiaji wa dawa za kulevya na kupunguza
maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Amesema taasisi hiyo ambayo inafanya kazi kwa karibu na kituo cha
kudhibiti maradhi mbali mbali nchini Tanzania (CDC), ni vyema ikafikiria
namna ya kuleta huduma zao hapa Zanzibar, ili kusaidia kupunguza
maambukizi ya Ukimwi hasa kwa makundi hatarishi yakiwemo ya watumiaji wa
dawa za kulevya.
Amesema Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi mbali mbali za kudhibiti
uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kuimarisha
ulinzi, sambamba na kuanzishwa kwa Sober houses ambazo zimekuwa
zikiwasaida vijana walioamua kuachana na matumizi ya dawa hizo.
Kwa upande wake wao wataalamu hao kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani
wamesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni muhimu katika
kukabiliana na maradhi mbali mbali yakiwemo Ukimwi.
Wamesema taasisi hiyo imeanza kupata mafanikio makubwa kwa upande wa
Tanzania Bara ambapo wamekuwa wakisaidia kutoa ushauri na dawa za
Methadone ambazo huwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga
sindano kuweza kupunguza athari za dawa hizo.
Wamesema kufika kwao Zanzibar ni hatua ya matayarisho ya awali ya
kuweza kufikisha huduma hizo hapa nchini, na kwamba hatua nyingine zaidi
zitafuata katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inanufaika na huduma hizo
zikiwemo utoaji wa tiba ya Methadone kwa watumiaji wa dawa za kulevya.
Mapema akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi huo, Mkurugenzi wa Tume ya
kuratibu ya udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar Bwana Ahmed Salim Awadh
amesema tayari zipo program mbali mbali zinazolenga kuwafikia moja kwa
moja watumiaji wa dawa za kulevya, ili kupunguza athari kwa watumiaji
hao.
Amesema tume yake kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, inakusudia
kushirikiana na taasisti hiyo ya Pangaea ya Marekani ili kuhakikisha
kuwa watumiaji wa dawa za kulevya na waathirika wa Ukimwi wanapatiwa
tiba mbadala na kuweza kupunguza athari zitokanazo na majanga hayo.
Mkurugenzi huyo amesema kwa sasa wanajiandaa kuupokea mradi huo, na
kwamba hatua za awali zitakuwa ni kuwaandaa watoaji wa huduma ili kuwapa
taaluma na kuweza kuwafikia walengwa kwa urahisi.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)