MALINZI AVUNJA UKIMYA AKIZINDUA ROCK CITY MARATHON 2012 - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MALINZI AVUNJA UKIMYA AKIZINDUA ROCK CITY MARATHON 2012

 Mwenyekiti wa Baraza la Michezo nchini (BMT) Dioniz Malinzi akiongea na waandishi wa habari kwenye hafla ya uzinduzi wa mbio za nne za Rock City Marathon 2012 zitakazofanyika Oktoba 28 jijini Mwanza
 Picha tofauti za wawakilishi wa Makampuni na Mashirika yanayodhamini mbio za Rock City Marathon 2012, wakizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mbio hizo kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam leo mchana
 Wawakilishi wa Makampuni na Mashirika yanayodhamini mashindano ya mbio za Rock City Marathon 2012, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa mbio hizo kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam leo

 Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Riadha Tanzania, Tullo Chambo (wa pili kushoto), akifuatilia uzinduzi wa Rock City Marathon 2012 akiwa pamoja na Mweka Hazina wa RT, Suleiman Is Haq (mwenye shati jeupe) kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam leo.

DAR ES SALAAM, Tanzania

JITIHADA za wazi baina ya serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), vyama vya michezo, mashirika na wadau wengine zinahitajika, ili kurejesha heshima iliyopotea miongoni mwa michezo na wanamichezo wa Tanzania, hususani riadha.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo na Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mbio za Rock City Marathon 2012 uliofanyika kwenye Hoteli ya New Africa. 

Malinzi alisema kuwa, kama Mwenyekiti wa BMT, anatambua kudorora kwa michezo hasa riadha nchini, hali iliyotokana na vyama kujaza ‘wachumia tumbo’ katika nyadhifa zake, jambo linalochangia ukosefu wa changamoto mpya za maendeleo.

“Michezo imedorora na kimsingi inatia aibu. Taifa kama hili lenye watu zaidi ya milioni 40 kuwakilishwa na watu sita katika Olimpiki 2012. Wanachofanya wenye dhamana kwenye vyama ni ufisadi, unaopaswa kukomeshwa sasa, ikiwa tunataka kupata maendeleo ya michezo,” alisema Malinzi.

Aliongeza kuwa, BMT imefurahishwa na mafanikio waliyopata waandaaji wa Rock City Marathon, kampuni ya Capital Plus katika kuendesha mbio hizo kwa mwaka wa nne na kuwa, baraza lake liko tayari kutoa kila aina ya ushirikiano kwa kampuni hiyo na nyingine kufanikisha matukio yenye nia ya kulipa heshima taifa kupitia michezo.

Alisisitiza kuwa, aibu ya kuvurunda Olimpiki 2012 ni ya kujitakia, kutokana na kuona ufisadi bila kuchukua hatua katika vyama vya michezo, huku viongozi wake wakiwekeza katika kujijengea majumba ya kifahari na kuacha michezo husika ikikosa dira.
 
Malinzi, alienda mbali zaidi na kuzungumzia hatua ilizochukua BMT, baada ya kubaini ubabaishaji mkubwa katika Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), ambako viongozi waliokuwepo walikuwa wakipitisha muda wao wa kukaa madarakani makusudi, ambako walifanikiwa kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi kwa mbinde ambao umeleta changamoto mpya.

Aligeukia mashirika na vyama vya michezo, vinavyokumbatia mashindano na matukio yasiyo na tija kwa michezo na wanamichezo na kutaka vita dhidi ya taasisi za aina hiyo kuwa kali, ili kurejesha heshima ya riadha, mchezo uliyoipa Tanzania sifa kubwa nje ya mipaka.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Capital Plus, Dk. Ellen Otaru Okoedion, alisema kuwa, Rock City Marathon (RCM), inatarajiwa kufanyika Oktoba 28 jijini Mwanza na kuwa, kampuni yake inajivunia mafanikio yaliyopatikana kwa miaka minne.

Alisema RCM 2012 itakuwa chini ya kaulimbiu; ‘Utalii Kupitia Michezo’, sera itakayosaidia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii.

Mbio hizo zinadhaminiwa na PPF, NSSF, TTB, TANAPA, Geita Gold Mine, African Barrick Gold, Air Tanzania, Sahara Communications, Nyanza Bottlers, Airtel Tanzania, New Mwanza Hotel, New Africa Hotel na zitashirikisha wanariadha wa rika tofauti kuanzia watoto hadi watu wazima.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages