Wanasheria wa
serikali wakiwasili mahakama kuu divisheni ya kazi jijini Dar es Salaam
Alhamisi, Agosti 2, 2012 kusikiliza uamuzi wa mahakama hiyo.
Rais wa Chama cha Walimu nchini (CWT), Gratian Mukoba, akiingia mahakamani Agosti 2, 2012
Katibu Mkuu wa chama cha Walimu nchini (CWT), Ezekiel Oluoch, akiwasili mahakamani hapo Alhamisi Agosti 2, 2012
Wanasheria wa serikali wakisubiri uamuzi wa mahakama Alhamisi Agosti 2012
Viongozi wa vyama vya wafanyakazi, pamoja na walimu, wakiwa mahakamani Alhamisi Agosti 2012, kusubiri uamuzi huo wa mahakama
Viongozi wa
vyama vya wafanyakazi pamoja na walimu, wakiwasili mahakama kuu
divisheni ya kazi barabara ya Bibi Titi Mohammed jijini Dar es Salaam
alhamisi Agosti 2, 2012 kusikiliza uamuzi wa mahakama kuhusu hatma ya
mgomo wa walimu nchini Tanzania
Polisi wakilinda usalama nje ya mahakama.Picha na Mdau Khalfan Said
--
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Kazi jijini Dar es Salaam, imesema mgomo wa
walimu ni batili kwasababu haukuzingatia matakwa ya kifungu cha
84(1),(2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazi ya mwaka 2004 na
uliandaliwa kwa dhamila mbaya.
Jaji Sophia Wambura wa mahakama hiyo alitoa uamuzi huo jana saa 9:14-37
alasiri huku ukumbi wa wazi wa mahakama hiyo ukiwa umefurika walimu
ambapo katika uamuzi wake huo pia aliwataka walimu wote kurejea mara
moja kazini.
Jaji Wambura alisema asikiliza kwa makini hoja za mawakili waandamizi wa
serikali Pius Mboya na Obadia Kameya ambao walikuwa wakiwawakilisha
walalamikaji katika maombi hayo madogo namba 96/2012 yaliyoletwa chini
ya hati ya dharula na Katibu Mkuu Kiongozi,Katibu Mkuu Ofisi ya rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ya
mdaiwa ambaye ni Chama cha Walimu Tanzania(CWT) ambao walikuwa
wakiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Gabriel Mnyele.
Jaji Wambura alisema mgogoro uliowasilishwa mbele yake na walalamikaji
ni kwamba wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa mgomo wa walimu ni batili
wakati wakili wa CWT ,Mnyere alidai mgomo huo ni halali kwa sababu
umekidhi matakwa ya sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.
Jaji huyo alisema mahakama yake imefikia uamuzi wa kutofautiana na
zoezi la upigaji kura za kuunga mkono mgomo ambalo liliendeshwa na CWT
ambapo asilimia 97 ya walimu waliinga mkono kuanza kwa mgomo kwasababu
zifuatazo:
“Mosi, zoezi lile la upigaji kula lilikuwa likiwadanganya wanachama wa
CWT kuwa zoezi hilo limeendeshwa rasmi na kwa mujibu wa sheria,zoezi
lile halikukidhi matakwa ya sheria kwasababu wanachama wake walikuwa
hawajaelewa na viongozi wa chama hicho madhara ya kufanya mgomo
huo,zoezi lile halikufuata taratibu;
“Noti ya kugoma iliyotolewa na CWT Julai 27 mwaka huu saa tisa alasiri
wakati zoezi la upigaji kura zile lilikuwa bado halijafanyika na
kwasababu hiyo zoezi lile likikuwa batili:
“Kwa mdaiwa(CWT) kushindwa kufuata matakwa ya kifungu cha 42 na 43 cha
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini,ni wazi taratibu zote walizozifanya
za kupiga kura ya kuunga mkono mgomo na kugoma mdaiwa alizifanya akiwa
na dhamila mbaya kwani wajumbe wa chama hicho hakuwa na makubaliano ya
jinsi mgomo utakavyoendeshwa na kusimamiwa”alisema Jaji Wambura huku
baadhi ya walimu wakiwa wamejiinamia.
Alisisitiza kuwa CWT imeitisha mgomo huo ikiwa na dhamira mbaya
kwasababu ni CWT ndiyo alikataa kuendelea na mazungumzo na mwajiri wake
badala yake akaanzisha mgomo wakati Julai 27 mwaka huu, pande zote
katika hizo zilifika mbele yake kuomba na upande wa mlalamikaji ukaomba
mahakama itoe amri ya kutaka pande zote zisiendelee na jambo lolote hadi
mahakama itakapowasilikiliza lakini cha kushangaza siku hiyo hiyo saa
tisa alasiri CWT ilienda kutoa noti ya kuanza mgomo kwa walimu nchi
nzima ndani ya saa 48 wakati kulikuwa na amri ya mahakama iliyozitaka
pande zote kutoendelea kufanya jambo lolote linalohusiana na kesi hiyo
ambapo mgomo huo batili ulianza rasmi nchi nzima kuanzia Jumatatu ya
wiki hii na hadi sasa unaendelea.
“Kwa maelezo hayo hapo juu nasisitiza mgomo huo ni batili kwani
haujakidhi matakwa ya kifungu cha 84(1),(2) cha Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini ya mwaka,na mgomo uliondeshwa kwa siku tatu sasa ni
batili na ninaamuru mgomo huo usitishwe mara moja na walimu wote
warejee kazini na kwa kuwa mdaiwa aliitisha mgomo huo kwa mkutumia
taarifa kwa vyombo vya habari pia naamuru kiongozi aliyetoa taarifa hiyo
ya mgomo aende tena kwenye vyombo vya habari akatangaze kuwa mgomo
waliokuwa wakiufanya ni batili na kuwataka walimu warejee kazini mara
moja na mahakama hii imemshangaa sana wakili Mnyere kwa kushindwa
kuwashauri wateja wake mapema kwamba mgomo waliokuwa wakiundesha ulikuwa
umekiuka sheria” alisema Jaji Wambura.
Aidha pia naiamuru CWT kulipa gharama na fidia kwa kipindi chote
ambacho wanafunzi wamekosa vipindi kwaajili ya mgomo huo batili na kama
pande zote zinaona kuna hata ya kurudi meza ya majadiliano zilirudi
kwenye meza ya majadiliano na zimualike mtaalamu wa sheria za kazi
awasaidie kufikia mwafaka.
Baada ya hukumu kutolewa,baadhi ya viongozi wa CWT waliwaomba waandishi
wa habari waje nje ya mahakama kwani kutakuwa na mkutano lakini hata
hivyo waandishi walipofika nje ya viwanja hivyo mahakama walimkuta Rais
wa chama cha walimu,Gration Mkoba akiwa amenyongonyea na hata
alipotakiwa atoe tamko ni lini atatekeleza amri ya mahakama iliyomtaka
aende kwenye vyombo vya habari autangazie umma kuwa mgomo alioutisha ni
batili na awatake walimu warudi kazini alishia kusema leo atafanya
mkutano na waandishi wa habari na kwa upande wa wakili wao Mnyere
alisema amekubaliana na uamuzi huo wa mahakama.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)