Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa Nchini Tanzania Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Baloi Seif Ali Iddi akikiendesha Kikao cha
Saba cha Kamati hiyo kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu Mjini
Dar es slaam.
Wajumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa Tanzania Dr. Herison Mwakiembe
na Mh. January Makamba wakiendelea na Kikao chao cha saba cha Kamati
hiyo katika Ofisi ya Waziri Mkuu Mjini Dar es salaam.
Baadhi
ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa Tanzania Mh.Sophia simba na
Hajat Amina Mrisho wakifuatilia mijadala ya Kikao hicho
kilichofanyika Mjini Dar es salaam.
--
Kikao cha saba cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya
Mwaka 2012 Nchini kimekutana leo mjini Dar es salaamu kutathmini zoezi
la kuhesabu Watu lililoanza usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita ya
Tarehe 26/8/2012.
Wajumbe wa Kikao hicho walikutana katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu
wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dar es salaam
chini ya Mwenyekiti Mwenza wa Kikao hicho Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Akitoa Taarifa katika kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Albina Chuwa alisema
hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya Watu waliokataa
kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu naMakazi pamoja na uandikishaji
wa Vitambulisho wa Uraia.
Dr. Alibina alisema Ofisi ya Takwimu ya Taifa ilizipatia Ofisi ya
Polisi za Mikoa sheria na kanuni za Takwimu zinazoelezea kwa ufasaha
haki za Mwananchi zinazompasa kujiandikisha kwenye zoezi la Sensa pamoja
na zile zinazomkabili endapo atakataa kuhesabiwa.
Alisema hatua hiyo ililenga kurahisisha utekelezaji wa sheria hiyo
ndani ya kipindi cha zoezi zima la kuhesabu Watu katika kipindi hichi
cha Sensa ya Watu na Makazi yam aka 2012.
Kwa upande wao Mawaziri wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
na Ile ya Mapinduzi ya Zanzibar walisema jitihada zimechukuliwa katika
kuipatia madodoso Mikoa ambayo ilikumbwa na upungufu wa Vifaa hivyo.
Walisema hatua hiyo ya haraka imefanywa ili kuona zoezi la hesabu ya
watu na makazi na uandikishaji wa Vitambulisho vya uraia linamalizika
kwa kwa mafanikio kama lilivyopangwa.
Walifahamisha kwamba jumla ya shilingi Bilioni 22.8 awamu ya kwanza
tayari zimeshapelekwa Mikoani kwa ajili ya wasimamizi na Makarani wa
sensa na shilingi Bilioni 22.8 nyengine zitatolewa kabla ya Tarehe
30/8/2012.
Aidha walizielezea baadhi ya changamoto zilizojichomoza ndani ya zoezi
hilo ikiwemo baadhi ya watu katika shehia miongoni mwa hizo ni pamoja na
Chwaka,kilindi, Nungwi,Pangawe, Fundo, Kilwa na Lindi.
Halkadhalika Mawaziri hao waliwanasihi Wananchi kwamba kila mwana Jamii
anahakikisha anafanikisha zoezi zima la sensa ya Watu na Makazi Hapa
Nchini.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na
Makazi Tanzania ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi alivipongeza Vyombo vya Habari Nchini kwa juhudi
ilivyochukuwa ya Kuhamasisha pamoja na kutoa Elimu kwa Umma juu ya
umuhimu wa Sensa a Watu.
Balozi Seif alifahamisha kwamba ujumbe na Taaluma hiyo kwa kiasi
kikubwa imewafikia Wananchi kwa asilimia kubwa kama ilivyotarajiwa.
“ Waliokataa kuhesabiwa kwenye zoezi hilo la
kuhesabu watu kwa kweli wana lao”. Alielezea Mwenyekiti huyo Mwenza wa
Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa Nchini.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)