WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina
Kombani amesema Serikali haiwezi kulipa kima cha chini cha mshahara cha
Sh 315,000 kilichopendekezwa, kwani kufanya hivyo kutailazimu kutumia
asilimia 60 ya Bajeti yake kwa mishahara tu.
Alisema hayo jana bungeni wakati akitoa majumuisho ya makadirio ya
matumizi ya Wizara yake, akiongeza kuwa jambo hilo halitekelezeki, bali
Serikali itaendelea kuboresha mishahara ya watumishi wa umma kadri fedha
zitakavyopatikana.
Kuhusu motisha kwa wafanyakazi, Kombani alisema kila kada kwenye
utumishi ipo inayofanya kazi kwenye mazingira magumu na kwamba motisha
itaangaliwa na kutolewa kwa wote bila kuangalia watumishi wa maeneo ya
pembezoni pekee.
Mbali na hayo, Kombani pia alitaka wabunge kuchunga ndimi zao
wanapochangia mijadala na kutoa hoja bungeni ili wasimamie vizuri
sheria, kwani kuendelea kushawishi watumishi kugoma si suluhu ya
matatizo.
“Nakuombeni wabunge mkumbuke, kwamba wajibu wenu ni kusimamia sheria,
pia chungeni ndimi zenu, mnaweza kutamka jambo likawa baya, si vyema
kuwaambia watumishi waendelee kugoma, maana kufanya hivyo si suluhu,”
alisema Kombani.
Kuhusu ukubwa wa Serikali, alisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya
kupanga ukubwa wa Serikali yake na pia upangaji huo huzingatia vigezo
zinavyohitajika, vikiwamo vya ukubwa wa nchi, idadi ya watu na kuangalia
uwiano wa pato la nchi.
Alisema kuhusu pato, uwiano unaotakiwa ni asilimia 17 hadi 35
kutumika kulipa mishahara na kwa upande wa Serikali ni asilimia 27.1,
hivyo bado nchi iko kwenye kiwango kizuri cha ukubwa wa Serikali.
“Tanzania haina Serikali kubwa, kiwango cha mapato na matumizi ya
nchi ni asilimia 27.1, sasa utaona hata hatujazidi, kwani tunatakiwa
kuwa kati ya asilimia 17 hadi 35, na sisi tuko 27.1, nchi nyingine za
Afrika na hata Afrika Mashariki zimevuka kiwango chetu, ingawa pia wao
wana idadi ndogo ya watu na eneo dogo,” alifafanua Kombani.
Akizungumzia suala la watumishi hewa, Kombani alisema hilo linatokana
na watumishi halali walioondolewa kwenye orodha ya malipo kuendelea
kulipwa isivyo halali.
Alisema Serikali imebaini kuwapo watumishi hewa na hadi sasa
watumishi 12,000 wameondolewa kwenye orodha ya malipo na kwamba wengine
5,745 wamepewa adhabu ya nidhamu. Hata hivyo, alisema watendaji waliohusika kwenye suala la watumishi
hewa wamechukuliwa hatua, wakiwamo watuhumiwa sita ambao wamefikishwa
mahakamani na pia majalada 86 ya watuhumiwa yako mahakamani kwa hatua za
kisheria.
Akihitimisha mjadala wa Ofisi ya Rais Utawala Bora, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Utawala Bora, George Mkuchika, alisema Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), haiwezi kulisafisha Bunge na tuhuma
za rushwa, bali wenye jukumu la kufanya hivyo ni wabunge wenyewe.
“Wabunge wenyewe ndio wenye wajibu wa kujisafisha, kazi hiyo si ya
Takukuru, tunapaswa kujisafisha tuhakikishe hakuna rushwa miongoni
mwetu,“ alisema Mkuchika.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)