Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Mhe Said Ali
Mbarouk, akizungumza na ujumbe wa Wafanyakazi wa TV Oman ulipofika
ofisini kwake kujitambulisha kwa ujio wao Zanzibar wa kutengeneza
Program ya Utalii wa Zanzibar na Majumba ya Mji Mkongwe na sehemu za
Historia ya Zanzibar kuitangaza Kitalii Oman, kushoto kwa Waziri Balozi
wa Oman Zanzibar Mansoor Al Busaid na Wafanyakazi wa TV Oman.
Balozi wa Oman Zanzibar Mansoor Al Busaid, akizungumza na Waziri wa
Habari Utamaduni Utalii na Michezo walipofika Ofisini kwake kutambulisha
Ujumbe wa TV Oman uliofika Zanzibar kwa ajili ya kufanya program
mbalimbali za historia na kuitangaza Zanzibar Kitalii Nchini Oman.
Balozi wa Oman Zanzibar Mansoor Al Busaid, akizungumza na Waziri wa
Habari Utamaduni Utalii na Michezo Mhe Said Ali Mbarouk, alipofika
Wizarani kuwatambulisha Wafanyakazi wa Oman kufanya program mbalimbali
za kuitangaza Zanzibar Kitalii nchini Oman.
Wafanyakazi wa TV Oman wakiwa katika mazungumzo na Waziri wa Habari Ofisini kwake walipofika kujutambulisha.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Mhe.Bihindi Hamad,
Mkurugenzi Mipango na Uendeshaji Joseph Kilangi na Mtayarishaji wa
Vipindi wa ZBC TV Ahmeid Talibm wakisikiliza Waziri wakati wa mkutano
huo. uliofanyika katika Ofisi ya Wizara ya Habari Kikwajuni.
---
UONGOZI wa Shirika la Utangazaji nchini Oman, umeahidi kulisaidia
Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC – TV) katika nyanja mbali mbali,
ikiwemo za kiufundi na kitaaluma, ili liweze kuharakisha juhudi zake za
kutoka kwenye mfumo wa Teknolojia ya habari wa Analogy na kuelekea ule
wa Digital.
Ahadi hiyo imetolewa jana na Uongozi wa Shirika hilo, wakati ulipokutana
na kubadilishana mawazo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk, ofisini kwake Mnazi Mmoja.
Ujumbe huo wenye timu ya waandaji wa filamu, upo nchini kwa ajili ya
kutayarisha filamu katika maeneo ya kihistoria, hususan Mji Mkongwe,
ambapo pamoja mambo na mengine filamu hiyo itaisaidia kuitangaza
Zanzibar kiutalii.
Ujumbe huo ambao uliambatana na Balozi mdogo wa Oman nchini, Mansoor Al
Busaid, umeahidi kukutana na Menejment ya ZBC, ili kubadilishana uzoefu
pamoja na kuangalia maeneo yepi ambapo Shirika hilo linaweza kusaidia
kiufundi na kitaaluma.
Mmoja wa viongozi wa Shirika hilo, Ebrahim Al Yahmad alisema ZBC inaweza
kunufaika sana kuwepo mashirikiano na Shirika hilo na kuharakisha
safari yake ya kuelekea Digital,kwa kuzingatia kuwa tayari Oman
inaondoka katika mfumo huo (Digital ) na kuelekea mfumo wa DH.
Alisema Shirika la Utangazaji la Oman, (ambalo lina Waziri wake)
limepiga hatua kubwa sana katika nyanja ya mawasiliano ya habari, hivi
sasa likiwa tayari limejenga Studio kubwa ya kisasa, huku likiendelea na
maandalizi ya program za mafunzo kwa mfumo wa DH.
Alisema katika dhana ya kuendeleza mashirikiano kati ya mashirika hayo
mawili, vijana wa Zanzibar wataweza kupata fursa ya kubadilishana uzoefu
na wenzao wa Oman na kuona vipi wanafanya kazi.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo alisema hatua ya kuja kwao nchini
na kuandaa filamu katika maeneo ya kihistora kutaisaidia sana kuutangaza
Utalii wa Zanzibar, kwa kujua kuwa Zanzibar ni eneo bora kwa biashara
ya Utalii.
Aidha alimwomba Waziri Mbarouk kusaidia upatikanaji wa nakala za
magazeti ya zamani ambayo yaliwahi kuchapishwa hapa nchini, au kumpata
mtu ambae anaweza kueleza kwa ufasaha juu ya uwepo wa magazeti hayo.
Mapema Waziri Mbarouk alisema Serrikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko
tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na ndugu zao wa
Oman.
Alisema hatua ya Oman TV kuja nchini kwa ajili ya kuandaa filamu maalum
katika maeneo ya kihistoria, ni hatua muafaka inayounga mkono juhudi za
Serikali katika kuutangaza utalii wa Zanzibar hadi nje ya mipaka na
kufanikisha ‘dhana ya utalii kwa wote’.
Alisema mbali na ujumbe huo kuangalia eneo la Mji Mkongwe, pia wapaswa
kuangalia maeneo zaidi ya kihistoria, ikiwemo msitu wa Jozani, magofu ya
Mtoni, fukwe zenye kupendeza pamoja na magofu ya Mazrui yalioko Chwaka
kijiji cha Tumbe, kisiwani Pemba.
Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii, na kutoa
mfano wa Hifadhi yam situ wa Jozani, wenye kupatikana Kima Punju,
wanyama ambao hawezi kupatikana mahala popote pale Duniani, isipokuwa
Zanzibar.
Aidha aliyasifia magofu yalioko Chwaka Tumbe, kwa kusema kuwa ni eneo
kubwa, linalovutia na lenye historia inayosisimua, likielezwa kuwa ni
mji uliopata kuishi watu kutoka Oman kabla ya kuja kwa Wareno.
Akizungumzia kuwepo kwa magazeti ya zamani, Mbarouk alisema kuna idadi
kubwa ya magazeti yaliokuwa yakichapishwa hapa Zanzibar miaka mingi
iliopita, na kuuahidi ujumbe huo kupata baadhi ya nakala zake pamoja na
watu wanaoelewa historia ya kuwepo kwa magazeti hayo.
Na
Abdi Shamnah -
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)