Na Mwandishi Wetu
WAREMBO
12 wanaotarajia kuwania taji la kitongoji cha Kigamboni mwaka huu 'Miss
Kigamboni City 2012' leo Jumatano wanatarajiwa kufanyiwa usaili kwa
ajili ya kuanza safari ya kumpata mshindi wa shindano hilo
litakalofanyika Ijumaa kwenye ukumbi wa Navy Beach jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa shindano hilo, kutoka
kampuni ya K&L Media Solutions, Somoe Ng'itu, alisema jana kuwa
maandalizi ya zoezi hilo yamekamilika na wanachosubiri ni siku ya
shindano ifike.
Alisema kuwa kitongoji hicho kina
warembo wenye sifa na wanaojiamini ambao wamepania kurudisha taji la
Miss Tanzania kwenye Kanda ya Temeke.
Aliongeza kuwa ili kuboresha shindano
hilo bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma
na msanii na mchekeshaji mahiri hapa nchini, Mpoki watatumbuiza kwenye
kinyang'anyiro hicho.
"Tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo
kufika kushuhudia mrembo wa Kigamboni atakavyopatikana, ni Kitongoji
kilichoko sehemu pekee hapa nchini na kulikosa kushuhudia itakuwa ni
kujinyima burudani wewe mwenyewe," alisema mratibu huyo.
Aliwataja warembo watakaochuana kuwa
ni pamoja na Susanne Jeremiah, Agness Goodluck, Elizabeth Boniface,
Dorothea Kessy, Esther Albert, Edda Silyvester, Sophia Martin, Doreen
Kweka, Khadija Kombo, Linnah David, Rosemary Peter na Winnie Karaya.
Aliwashukuru wadhamini ambao
wamejitokeza kusaidia shindano hilo ambao ni Redd's, Dodoma Wine, hoteli
ya Hope Country, Screen Masters, Global Publishers, Nobro Collections,
Times FM na Clouds FM.
Aliongeza kuwa warembo watakaoshika
nafasi tatu za juu kutoka katika shindano hilo wataungana na wenzao
kutoka vitongoji vya Kurasini na Chang'ombe ili kuwania taji la Kanda ya
Temeke baadaye mwaka huu.
|
-
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)