Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Masagala nje kidogo ya Mji mdogo wa
Maganzo, akitoka kuchota maji bwawani, bwawa hili lilichibwa na
mkandarasi aliyekuwa akitengeneza barabara kwa matumizi ya ujeni.
Lwinzi Kidiga, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Maganzo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Maganzo, Lwinzi Kidiga.
Binti akichota maji katika moja ya mabwawa ambayo si salama kwa
matumizi anuai, bwawa hili lilichibwa na mkandarasi aliyekuwa
akitengeneza barabara kwa matumizi ya ujeni.
Mabinti wakitoka kusaka maji kwa matumizi anuai.
Binti akichota maji katika moja ya mabwawa ambayo si salama kwa
matumizi anuai, bwawa hili lilichibwa na mkandarasi aliyekuwa
akitengeneza barabara kwa matumizi ya ujeni.
--
Na Joachim Mushi,
SHIDA ya maji inayoikabili Wilaya ya Kishapu imeendelea
kuwabebesha wananchi mzigo pasipo kutarajia, hasa wagonjwa kwani kwa sasa
wananchi wa Mji mdogo wa Maganzo Kata ya Songwa wanalazimika kwenda kutibiwa
wakiwa na madumu ya maji kulingana na huduma anayoita muhusika.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi mjini hapa,
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Maganzo, Lwinzi Kidiga alisema
wamewaelekeza wananchi kwenda kutibiwa huku wakiwa na maji kwenye madumu ili
kuiwezesha Zahanati ya Maganzo kuendesha shughuli zake kwani hakuna maji katika
kituo hicho.
Alisema wananchi eneo hilo
hulazimika kwenda na maji kati ya madumu (ya lita 20) mawili hadi matatu kulingana
na uhitaji wa maji katika huduma ambayo mgonjwa anastahili kupata jambo ambalo
amekiri kuwa ni kero kwa wananchi wake.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini
licha ya wananchi kulazimika kuja na maji katika zahanati hiyo pia wanapokuja
kupata huduma za afya usiku hulazimika pia kuja na mafuta ya taa au tochi
ambayo hutumika kuangaza wakati mgonjwa akipatiwa huduma, kwani zahanati hiyo
haina umeme.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Lucas
Said akizungumza na mwandishi wa habari hizi amekiri kuwepo na utaratibu wa
kuwatoza maji wananchi wanaokwenda kupata huduma za afya na kudai tatizo la
maji lipo kwa zahanati nyingi za eneo hilo na juhudi zinafanywa kuhakikisha
huduma ya maji inapatikana maeneo anuai ya Kishapu.
Alisema kwa sasa wataalamu wanafanya utafiti katika vijiji
mbalimbali kuhakikisha vinapatiwa huduma ya maji pale mpango wa kuleta maji
kutoka Ziwa Victoria kwa matumizi eneo hilo utakapo kamilika.
Hata hivyo ameshauri watendaji katika zahanati na vituo vya afya kuhakikisha
wanajipanga vizuri katika matumizi ya fedha za ruzuku ili ziweze kugharamia
huduma kama hizo na kuondoa usumbufu kwa
wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Maganzo, Kidiga ilipo
zahanati hiyo amesema tayari uongozi wa kijiji umefanya mazungumzo na mwekezaji
wa madini ya almasi eneo hilo, mmiliki wa mgodi
wa Williamson unaochimba almasi eneo hilo
kuwaletea maji wananchi mradi utakaoanza kati ya mwezi Julai mwaka huu.
*Habari hii
imeandaliwa na kuletwa hapa na Mtandao wa www.thehabari.com kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)