Mbunge
wa Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel, akiwa chini ya ulinzi wakati
alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es
Salaam leo kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili. Mbunge huyo
alikamatwa jana kwa kile kilichodaiwa kudai na kutaka kupokea Rushwa
baada ya kukamilika kwa mitego ya Wana TAKUKURU katika Hoteli ya Peacock
iliyopo maeneo ya Mnazi Mmoja jana.
Mbunge wa Bahi (CCM), Omary
Ahmed Badwel, akiwa chini ya ulinzi wa Polisi wakati akitoka Mahakamani
huku baada ya kusomewa mashitaka mawili ya rushwa ya sh. milioni 1,
aliyokuwa akiitaka kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mkuranga, Jonathan Liana.
Wakili wa Mbunge wa Bahi, Omary Ahmed Badwel, Mpare Mpoki (kushoto) akitoka Mahakamani.
Na Mwandishi Wetu, Jijini
MBUNGE
wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel (43) leo amefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kosa la rushwa ya shilingi Milioni
moja toka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan
Liana.
Wakili
wa Takukuru, Janeth Machullia na Ben Lincoln, walidai mbele ya Hakimu
Mkazi Faisal Kahamba, kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili
ya rushwa.
Wakili
Machullia, alidai kuwa kosa la kwanza ni la rushwa kinyume na kifungu
cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka
2007, kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu katika maeneo tofauti
jijini Dar es Salaam , Badwel, akiwa ni Mbunge wa Bahi na Mjumbe Kamati
ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na wakati huo akiwa ni ofisa wa
serikali kwa maana ya sheria ya Takukuru, alitenda kosa la kushawishi
ili apewe rushwa ya jumla ya Shilingi milioni nane kutoka kwa, Sipora
Liana, ili kiasi hicho cha fedha aweze kuwapelekea wajumbe wenzake wa
Kamati hiyo ya Bunge ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya mwaka
2011/2012 ya Halmashauri hiyo.
Wakili
Machullia, alidai shitaka la pili ni kwamba kati ya Juni 2 mwaka huu,
katika Hoteli ya Peacock, mshitakiwa akiwa na nyadhifa zake zote hizo
alipokea rushwa ya Milioni moja kutoka kwa Liana ili aweze kwenda
kuwashawishi wajumbe wa Kamati hiyo ili waweze kuipitisha ripoti ya
fedha ya Halmashauri ya Mkuranga huku akijua kufanya hivyo ni kosa.
Hata
hivyo mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki,
alikanusha mashitaka yote na wakili wa Machullia, alidai kuwa upelelezi
wa shauri hilo umekamilika.
Kwa
upande wake Hakimu Mkazi Kahamba, alisema ili mshitakiwa apate dhamana
ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atasaini
bondi ya shilingi milioni nne na kusalimisha hati zao za kusafiria
mahakamani, sharti ambalo lilitimizwa na mshitakiwa huyo na akapata
dhamana.
Hakimu
Kahamba, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu, kesi hiyo
itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuja kumsomea
maelezo ya awali mshitakiwa huyo.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)