Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
ameiwakilisha Tanzania katika mkutanano wa Mazingira Endelevu jijini Rio De
Janeiro unaofanyika jijini hapa ikiwa ni miaka 20 baada ya mkutano kama huo
kufanyika mwaka 1992. Katika mkutano wa mwaka 1992, ujumbe wa Tanzania
uliongozwa na Rais wa wakati huo Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Mkutano
wa mwaka huu unajadili kuhusu maazimio ya mwaka 1992 na namna yalivyotekelezwa
na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wapatao 182 huku washiriki katika mkutano
huu wakikadiriwa kutoka katika nchi 135. Sambamba na hilo mkutano huu unapitisha
maamuzi mapya kuhusu kuiweka dunia na mazingira yake katika hali ya usalama ili
yaweze kusaidia vizazi vijavyo. Mkutano huu unafanyika ikiwa ni siku chache
tangu kufanyika mkutano wa G-20 uliokuwa ukifanyika nchini Mexico na matokeo ya
mkutano huo wa G-20 kwa namna moja ama nyingine yameongeza hamasa ya mkutano
huu wa Rio +20. Hamasa kubwa kwa mataifa inabaki juu ya kutazama namna uchumi
wa kijani utakavyoweza kusaidia kukuza maendeleo ya maisha ya watu duniani huku
maendeleo hayo yakiiacha dunia katika hali ya kawaida katika mazingira yake ya
asili. Pia hoja ya kuhusu uzalishaji mkubwa wa gesi joto imepata mjadala mkubwa
katika mkutano huu. Maeneo mengine ambayo yanajadiliwa ni kuhusu hali ya
chakula duniani huku msukumo ukiwa kutoa uhuru kwa nchi kuzalisha chakula ili
kutosheleza wananchi wa kila nchi husika.
Ujumbe
wa Tanzania unaotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal unalenga
kuonesha namna Tanzania ilivyo na mikakati sadifu katika utunzaji wa mazingira yake
sambamba na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kikubwa
yanachangiwa na nchi kubwa zenye viwanda. Ujumbe huu pia unaakisi nafasi ya
nchi za Afrika katika kulinda mazingira pamoja na mikakati ya baadaye
inayozingatia uzalishaji bila kuathiri mazingira kwa kiasi kikubwa.
Katika
hotuba yake katika mkutano huu, Mheshimiwa Makamu wa Rais anazungumzia umuhimu
wa nchi duniani kuzidi kushikamana katika kuhakikisha dunia inabakia kuwa
sehemu bora ya kuishi kwa wanadamu wa sasa na wajao. Kufuatia mantiki hii,
Mheshimiwa Makamu wa Rais anayakumbusha mataifa yote kuhakikisha yanazingatia
maazimio ya mkutano huu wa Rio +20 ili uwe na mafanikio zaidi ya ule wa mwaka
1992.
Waliombatana
na Mheshimiwa Makamu wa Rais na ambao wanashiriki mikutano ya kisekta ni pamoja
na Mheshimiwa Terezya Huvisa, Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Fatma
Fereji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais SMZ pamoja na
Mheshimiwa Mahadhi J. Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa. Kundi la Wabunge linawakilishwa na Mheshimiwa James Lembeli, Salehe
Pamba na Magdalena Sakaya. Mkutano huu ulioanza Juni 20, 2012 unatarajiwa
kumalizika Juni 22, 2012.
Imetolewa na:
Boniphace Makene
Press Secretary to the Vice President
June 21, 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)