Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Mustafa Ali Garu,
akimuonesha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad namna chemchem inavyotiririka, katika chemchem ya Mtopepo
walipofanya ziara ya kutembelea chemchem hiyo jana tarehe 19/06/2012.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na
uongozi wa ZAWA wakiangalia upungufu wa maji katika eneo la Mtopepo
alipofanya ziara ya kutembelea chemchem ya Mtopepo jana. Kuliani kwake
ni Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdallah
Shaaban.Picha na Salmin Said-Ofisi Ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
---
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema
serikali italazimika kutumia ukali na kuondoa muhali kwa watu
wanaoendeleza vitendo vya uchafuzi wa mazingira hasa katika vianzio vya
maji.
Amesema ni hatari kuona vitendo hivyo vikiendelea huku taifa
likikabiliwa na uhaba wa maji unaotokana na uharibifu wa mazingira
katika vianzio hivyo.
Akiwa katika ziara ya kutembelea vianzio vya maji katika chemchem ya
Mtopepo, Maalim Seif ametahadharisha kuwa ikiwa vitendo hivyo vitaachiwa
kuendelea, kuna hatari ya taifa kuwa na upungufu mkubwa wa maji katika
miaka michache ijayo.
“Inabidi sasa tuwe wakali ili isije ikafika wakati tukawa hatuna maji katika nchi yetu”, alitahadharisha Maalim Seif.
Amesema katika kudhibiti hali hiyo, serikali itachukua kila aina ya
tahadhari kuhakikisha kuwa vianzio vya maji haviendelei kuharibiwa kwa
maslahi ya vizazi vijavyo na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya maji
Zanzibar (ZAWA) Dk. Mustafa Ali Garu amesema changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo kwa sasa ni uvamizi wa ujenzi karibu na vianzio vya
maji, hali inayopelekea mfumo wa uzalishaji wa maji kubadilika na
kupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha maji katika chemchem.
Kwa upande wake Mhandisi wa Mamlaka hiyo injinia Said Saleh amesema
baadhi ya chemchem ndogo ndogo zimeanza kutoweka, na kutaka tahadhari
zaidi zichukuliwe katika kudhibiti uvamizi wa vianzio hivyo.
Amefahamisha kuwa karibu nusu ya kiwango cha maji yamepungua katika
kipindi cha miaka kumi iliyopita kutoka katika chemchem za Mtotopepo na
Mwanyanya, huku chemchem ya Mtopepo ikiwa na upungufu mkubwa zaidi.Ziara
hiyo pia imemshirikisha Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe.
Ramadhan Abdallah Shaaban
Na
Na Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)