Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akitoa salaam
za pole kwa viongozi na chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa
Mwanza katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu
Musobi Mageni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiweka udongo kwenye kaburi la
Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu Musobi Mageni ,kulia kwake
ni Mwenyekiti wa Cuf Profesa ibrahim Lipumba ambao wote walijumuika
na viongozi na chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa Mwanza
katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu Musobi
Mageni
--
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amejumuika na
viongozi wa chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa Mwanza katika
mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu Musobi Mageni
huko kijijini kwao Ngudu, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Katika mazishi hayo, pia alihudhuria Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba, Makamu Mwenyekiti, Machano Khamis Ali, pamoja na
wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, wakiwemo Waziri wa Afya
Zanzibar, Juma Duni Haji na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Haki za
Binaadamu, Salum Bimani.
Marehemu Musobi alifariki Dunia Mei 30, mwaka huu nyumbani kwake Ngudu
baada ya kusumbuliwa na maradhi ya shinikizo na damu na sukari kwa muda
mrefu.
Marehemu alihamia chama cha Wananchi CUF mwaka 1994 na kuchaguliwa kuwa
Mwenyekiti Taifa mwaka 1995 hadi 1999 alipostaafu na kubaki kuwa
Mjumbe wa kudumu wa Baraza Kuu la Taifa na Mkutano Mkuu wa chama hicho
hadi kifo chake.
Katika uhai wake, marehemu aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo Mijini kuanzia mwaka 1972 hadi 1975, mwaka 1976 hadi 1978
Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Rajan Industries Ltd. Nafasi nyengine
ni alizowahi kushikilia ni Ubunge na Mkuu wa Wilaya katika wilaya ya
Chunya, Kahama na Muleba.
Akitoa salamu za rambirambi, Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye pia ni
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakati
wa mazishi alisema, marehemu alikuwa kisima cha busara na mwenye hekima
kubwa na ndio maana viongozi wa CUF walikuwa wakikimbilia kwake kuchota
ushauri wake.
“Huu ni msiba mkubwa sio tu kwa familia yake, bali kwa chama chetu na kwa serikali zote mbili”, alisema Maalim Seif.
Marehemu ambaye alizaliwa mwaka 1930, ameacha wajane wawili, watoto 15, wajukuu 28 na vitukuu sita.
Na
Khamis Haji
Ofisi Ya Makamu wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)