Ofisa Tabibu wa Kituo cha Afya Songwa, Bundala Nandule
Baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kama linavyoonekana pichani
Na Joachim Mushi, Thehabari.com-Kishapu
KITUO cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga kimekatiwa umeme kwa takribani miezi saba sasa kikidaiwa bili
ya umeme na TANESCO ya jumla ya sh. 38,000 hali inayowabebesha mzigo wa gharama
wananchi wanaofika kupata huduma kituoni hapo.
Wagonjwa wanautibiwa usiku katika kituo hicho hasa wanawake
wajawazito wanalazimika kugharamia mafuta ya taa kwenye chemli za kituo au
kuchangia sh. 1200 kabla ya huduma yoyoto ili kupatikana mwanga unaowawezesha
wahudumu kufanya kazi zao usiku.
Akizungumza na Thehabari.com juzi kijijini Songwa, Jamila
Nyalulu mkazi wa eneo hilo alisema wananchi
wasio na uwezo wa kuchangia mafuta ya taa hasa kwa huduma za uzazi wamekuwa
wakipata tabu, jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha yao kiafya.
Ofisa Tabibu wa Kituo hicho, Bundala Nandule amekiri hali
hiyo inakwamisha ufanisi wa utoaji huduma za afya hasa kwa wagonjwa wa usiku au
wanaopumzishwa na kuongeza kuwa tarari wameripoti suala hilo katika uongozi wa Halmashauri ya Kishapu
lakini bado linafanyiwa kazi.
“Tatizo la umeme linatusumbua kwa kweli hasa mgonjwa
anapokuja kupata huduma usiku. Wagonjwa wa kawaida hulazimika kuja na tochi,
lakini kwa wajawazito wanatakiwa kuja na fanta moja (chupa ya soda) ya mafuta
ya taa au aje na sh. 1200 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kabla ya huduma,”
alisema Nandule.
Hata hivyo akizungumzia tatizo hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kishapu,
Lucas Said alisema wanamshangaa Mkuu wa Kituo hicho cha afya kushindwa
kufuatilia malipo ya bili katika ofisi za halmashauri kwani cheki ya malipo ya
bili hiyo iliandikwa tangu mwaka jana (2011).
“Kituo hicho kilikuwa kinadaiwa sh. 38,000 na cheki
iliandikwa tangu mwaka jana lakini wahusika hawajatokea ili wakabidhiwe cheki
hiyo…huu ni uzembe,” alisema kiongozi huyo wa Halmashauri ya Kishapu.
Kituo cha afya cha Songwa kinatoa huduma kwa zaidi ya vijiji
vitatu vya Wilaya ya Kishapu, ambavyo ni pamoja na Kijiji cha Songwa, Bushola,
Seseko na baadhi ya zahanati zilizopo jirani na kituo hicho.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)