na Waandishi WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa LAAC, Iddi Azzan ameiomba Kamati hiyo
isihusishwe na tuhuma za mjumbe huyo za kukamatwa na Takukuru kwa tuhuma
za kupokea rushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Azzan alisema
Kamati hiyo imesikitishwa na kilichotokea na kujitoa kuwa haihusiki na
kitendo hicho cha Mbunge.
“Tumesikitishwa na kilichotokea, lakini ieleweke kuwa kila mtu
atalipwa kwa anachofanya, sisi Kamati yetu ina wajumbe 15 na tumekuwa
tukifanya kazi bila kuyumbishwa na mtu,” alisema Azzan.
Aliomba ieleweke, kuwa jambo lililotokea ni matatizo ya mtu binafsi
ambayo hayahusu Kamati hiyo. “Naomba na nasisitiza kuwa matatizo ya mtu
au uamuzi wake usihusishwe na Kamati … imekuwa ikifanya kazi kwa heshima
na kamwe haishurutishwi na mtu,” alisema.
Awali akizungumzia mapitio ya matumizi ya hesabu za Halmashauri ya Bagamoyo za mwaka 2009/10 na 2010/11, Azzan alisema Kamati hiyo ilikataa
kupokea hesabu za miradi miwili ya Mradi wa Maendeleo ya Kilimo
Wilayani (DADPS) na ya Mfuko wa Afya kutokana na mchanganuo mbovu wa
matumizi ya fedha zake.
Alitaka michanganuo ya miradi hiyo; wa DADPS wa Sh milioni 567 na
Mfuko wa Afya Sh milioni 570 iandikwe upya ikiwa ni pamoja na kuonesha
kuwa fedha hizo zimetumika kufanyia shughuli gani.
Yanusa ufisadi Aidha, aliitaka halmashauri hiyo pia kufanyia kazi
suala la matumizi ya Sh milioni 15 ambazo katika kitabu cha hesabu
zinaonekana zimetumika kununulia eneo la kujengea shule ya Zinga, wakati
Kamati hiyo ilipotembelea eneo hilo ilibaini kuwa eneo hilo lilitolewa
bure na wanakijiji wa Zinga.
“Hapa kuna namna haiwezekani fedha hizi zote zionekane zimetumika
kununulia eneo ambalo limetolewa bure na wanakijiji, Kamati inaagiza
halmashauri ilete majibu na kama zimeliwa, mhusika awajibishwe kwa
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Azzan.
Pia aliziagiza halmashauri zote nchini ambazo nyaraka zake ziko
mikononi mwa Polisi kwa ajili ya ushahidi, zihakikishe kabla ya
kupelekwa huko, nyaraka hizo zitolewe kivuli ili zitumike kwa matumizi
mengine ya halmashauri.
*Imeandikwa na Halima Mlacha na Flora Mwakasala
Chanzo: Habari Leo.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)