Hii ni nyumba ya moja ya kaya zilizotelekezwa na mwanaume kwa kisingizio cha kwenda kusaka maisha
Mhariri Mkuu wa Mtandao wa Thehabari.com, Joachim Mushi (wa kwanza
kulia) akifanya mahojiano na moja ya kaya za Kijiji cha Msasa hivi
karibuni Wilayani Handeni
Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani Handeni, Zawadi Gwando akifanya mahojiano na Thehabari.com
Na Joachim Mushi, Handeni
BAADHI ya wanaume wamelazimika kuzikimbia familia zao kwa
kisingizio cha ugumu wa maisha. Wanaume hao wamezitelekeza familia hizo na
kuziacha na wake zao na wao kutokomea maeneo mbalimbali kusaka maisha.
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni mjini hapa na mwandishi
wa habari hizi kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA)
umebaini kuwepo na familia nyingi ambazo zimetelekezwa na wanaume kwa
kisingizio cha kwenda kutafuta maisha maeneo mengine.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kwediyamba, Juma Abdul ambacho
ni moja ya vijiji vyenye idadi kubwa ya familia zilizotelekezwa, alisema matukio
ya utelekezaji familia kijijini hapo ni mengi na yamekuwa yakijitokeza kwa mitiozamo
tofauti.
Alisema kijiji hico kina kaya nyingi zilizotelekezwa na
wanaume, huku likiwepo kundi lingine la wanawake waliozaa watoto na wanaume
bila kufunga ndoa na baadaye wanaume kutoweka kwa madai wamekwenda kutafuta
maisha maeneo mengine.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kidereko, Shaban Muya alisema
matukio ya utelekezaji familia kwa kisingizio cha ugumu wa maisha hasa kwa
vijana wanaoingia kwenye ndoa ni mengi katika kijiji hicho jambo ambalo
limewalazimu kuanza kampeni ya kutaka wazazi wawawezeshe vijana wao wanapoingia
kwenye ndoa.
“Ofisi yetu imekuwa ikipokea malalamiko kama hayo mengi na
kuangalia namna ya kusuluhisha kulingana na imani zao…kama ni Waislamu yakitushinda
hupeleka Ofisi za BAKWATA mjini Handeni na kama ni Wakristu huangalia taratibu
za dini hiyo pia, lakini zipo familia zinatelekezwa ama wanatengana na wenza
wao na mwanamke anaendelea kuhudumia familia bila kulalamika, eneo kama hilo
viongozi hatuwezi kuingilia,” alisema Muya.
Vijiji ambavyo vimetembelewa na kushuhudia idadi kadhaa ya
familia zilizotelekezwa ni pamoja na Kwediyamba, Kivesa, Msasa, Komnyang’anyo, Kidereko,
Vibaoni na Kwachaga.
Naye Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani Handeni, Zawadi
Gwando, alisema kesi za malalamiko ya utelekezaji familia eneo hilo ni nyingi jambo
ambalo limeifanya idara hiyo kutumia muda mwingi kushughulikia migogoro ya
utelekezaji familia.
“Vitendo vya utelekezaji familia vipo vingi, kwa kutwa
unaweza kushinda ukipokea kesi za utelekezaji familia tu hadi mwisho wa
kazi...tatizo asilimia kubwa ya wakazi wa mji huu ni Waislamu ambao unakuta
wana wake zaidi ya mmoja...sasa inatokea mume anatelekeza baada ya kuona hali
ngumu ya maisha,” alisema.
Hata hivyo, Bi. Gwando ameshauri mamlaka za sheria kuangalia
upya sheria na adhabu zinazotolewa kwenye kesi za migogoro ya ndoa kwani adhabu
nyingi haziendani na wakati jambo ambalo huenda linawapa kiburi watuhumiwa wa
makosa kama hayo.
Uchunguzi umebaini baadhi ya watoto kutoka familia
zilizotelekezwa wameshindwa kuendelea na masomo hasa ya Sekondari kwa kile mama
kukosa kipato cha kutosha kuwasomesha watoto alioachiwa na mumewe.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)