Wanataaluma UDOM wakimbilia kwa JK - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Wanataaluma UDOM wakimbilia kwa JK


JUMUIYAya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), imemuandikia waraka Rais Jakaya Kikwete ikimuomba aingilie mgogoro baina yao na Uongozi wa Chuo wa Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kwa mujibu wa waraka huo wa Aprili 16, mwaka huu, jumuiya hiyo inadai mgogoro huo uliopo chuoni hapo unatokana na kufukuzwa kazi kwa baadhi ya wafanyakazi ambao ni wahadhiri.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Udomasa, Paul Loisulie alidai kuwa baada ya kutuma waraka huo kwa Rais Kikwete wanasubiri majibu.

“Rais ana njia nyingi za kujibu, pengine mabadiliko yakatokea…Mei 14 kuna kikao cha baraza la chuo na hapo tutajua hatima yetu na mambo yanaweza kuwa tofauti,” alisema Loisulie.

Waraka huo umeendelea kudai; “jumuiya ya wanataaluma imebidi iandike tena waraka huu kwa sababu mazingira yanavyoonesha, mgororo tulionao sasa tunachelea kusema kuwa ni visasi vilivyotokana na matokeo ya mgogoro ule wa mwanzo.”

Jumuiya inadai katika waraka huo kwamba mwishoni mwa 2011, kulikuwepo matukio ya kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi wa Udom hasa wanataaluma, tena kwa kunyemelewa na kushtukizwa, jambo walilodai kuwa ni ukiukwaji wa taratibu halali za Sheria ya Ajira.

Katika waraka huo, jumuiya hiyo imemuomba Rais Kikwete kuingilia kati kwa madai, hali inavyoonesha kuna fukuto kubwa linaloweza kusababisha mgogoro mkubwa zaidi ya uliokwisha tokea mwaka jana.

Januari mwaka jana, wahadhiri wa chuo hicho waligoma kufanyakazi kutokana na suala la maslahi yao, wakiushinikiza uongozi wa chuo utoe maelezo ya mishahara yao kutowafikia kwa wakati na mgomo ukakoma baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia kati na kuahidi kuyapatia ufumbuzi madai yao yote.

Wanaendelea kudai kuwa wahadhiri waliofukuzwa walipeleka malalamiko yao katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kupinga uamuzi wa kuwafukuza kazi kinyume cha sheria.

Aidha, wanadai baada ya majadiliano baina yao na menejimenti walikubaliana rufaa zao zirudishwe kwenye Kamati ya Rufaa ya Nidhamu kwa Wafanyakazi.

Kwa mujibu wa madai ya waraka huo, kamati ilimaliza kazi yake ambapo wanadai wahadhiri wanne walishinda rufaa hiyo, lakini uongozi wa chuo kupitia Baraza lake, uligoma na kuagiza kamati irudie kusikiliza rufaa hizo upya.

Wamedai kuwa hatua zilizochukuliwa na Udomasa baada ya kutoridhishwa, ililiandikia Baraza la Chuo kulitaarifu kuhusu ukiukwaji wa taratibu uliotokea na kuliomba liridhie taarifa ya uamuzi wa Kamati huru ya Rufaa za Wafanyakazi.

Pia jumuiya ilishauri kuwa kama menejimenti inahisi kutotendewa haki, ifuate taratibu za kisheria kudai haki yake.

“Sisi wanataaluma wa Udom, tumeonesha ustaarabu wa kuridhisha kwa kuwashauri wenzetu waliofukuzwa kufuata njia na taratibu za kisheria ya kudai haki zao kwenye vyombo vilivyoundwa kisheria kwa kukata rufaa badala ya kuingia kwenye mikutano au migomo.

Ustaarabu wetu huu bila shaka unapaswa kutambuliwa na yeyote mpenda haki na amani,” umeeleza waraka huo.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula alipozungumza jana, alisema Ijumaa iliyopita alikutana na Udomasa na kuzungumzia madai yao na kuyamaliza.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages