TAARIFA KWA UMMA
Mheshimiwa
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 4 Mei, 2012 alitangaza mabadiliko
katika safu ya Baraza la Mawaziri. Katika uteuzi wa Mawaziri na Manaibu
Waziri, Mheshimiwa Rais aliwateua Mawaziri wapya kutoka miongoni mwa
Wabunge aliokuwa amewateua na kuwatangaza. Baada ya uteuzi huo,
kumetolewa maoni kwamba hatua ya Mheshimiwa Rais kuwateua Wabunge Wapya
ambao hawajaapishwa Bungeni kuwa Mawaziri ni kitendo cha uvunjaji wa
Katiba.
Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayachukulia maoni haya kama ni jambo
lenye maslahi ya jamii na linalohitaji kufafanuliwa; kwa upande mmoja
lakini pia, kutolewa kwa elimu ya Umma; kuhusu Mamlaka ya Rais ya uteuzi
wa Wabunge.
Msingi wa Katiba tunaoanza nao ni maelekezo ya masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 55(4) kwamba: “Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge”
Pili,
ni mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge aliyopewa na masharti ya Ibara
ya 66(1)(e) yenye aina ya Wabunge wasiozidi kumi watakaoteuliwa na Rais
kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c)
za ibara ya 67 na angalau Wabunge watano kati yao wakiwa Wanawake.
Wabunge aliowateuwa Mheshimiwa Rais wanatokana na Ibara hii.
Tatu,
baada ya hatua zote hizi ikumbukwe kwamba aliyeteuliwa au kuchaguliwa
kuwa Mbunge anakuwa Mbunge ama baada ya kutangazwa na Msimamizi wa
Uchaguzi; au baada ya kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa wale Wabunge wa
viti maalum au anapochaguliwa na Baraza la Wawakilishi au anapoteuliwa
na Rais akitumia Mamlaka yake ya uteuzi yanayotokana na Ibara ya
66(1)(e). Hivyo Wabunge wanaohusika hawahitaji kuapishwa kwanza Bungeni
ili wawe Wabunge. Kiapo cha Mbunge Bungeni kinamwezesha tu kushiriki
katika shughuli za Bunge.
Katiba
ya nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua Mbunge wa
aina hiyo kuwa Waziri au Naibu Waziri Mbunge huyo awe ameapishwa Bungeni
kwanza. Masharti mawili muhimu na ya kuzingatia ni kwamba mteule wa
nafasi ya uwaziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka kwa
mujibu wa Ibara ya 56 ya Katiba, awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo
cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa
kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.
Sharti la pili, litahusu kiapo cha Uaminifu katika Bunge kabla Mbunge
hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge kwa masharti ya Ibara ya 68
ya Katiba. Viapo hivyo havitegemeani na vinaweza kufanyika kwa nyakati
tofauti.
Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inasisitiza kwamba Wabunge ambao
hawajaapishwa ndani ya Bunge ni Wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi
ya Uwaziri au Naibu Waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki
masharti yoyote ya Kikatiba au Sheria. Aidha, katika kutekeleza
madaraka ya kazi ya Uwaziri au Naibu Waziri Mbunge atahitaji kiapo mbele
ya Rais hata kama hajaapishwa Bungeni. Busara ya uandishi wa Katiba na
Sheria imetambua kwamba kunaweza kukatokea uteuzi wa aina hiyo wakati
Bunge limeahirishwa kama ilivyo sasa. Masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba
yatazingatiwa katika kikao cha Bunge kijacho.
Bila shaka ufafanuzi huu utaleta uelewa katika jambo hili na kuepusha mikangayiko isiyokuwa ya lazima.
Imetolewa na Jaji Frederick M. Werema (Mb)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
06 Mei, 2012






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)