MKE
wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda (pichani) amewashukuru Watanzania kwa
michango yao kwa ajili ya kuiandaa timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa
Queens) iweze kushiriki mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kuanza Mei
8-12, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ametoa
shukrani hizo leo mchana (Jumanne, Mei Mosi, 2012) wakati alipokuwa
akizungumza na wachezaji wa timu hiyo katika kambi yao iliyoko Shule ya
Filbert Bayi, Kibaha, mkoani Pwani. Mama Pinda ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Iwezeshe Taifa Queens Ishinde.
Mama
Pinda ambaye amewaongoza wake wa viongozi mbalimbali zaidi ya 20 ambao
ni wanachama wa New Millenium Group, alikabidhi katoni 40 za maji ya
kunywa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli (CHANETA), Bibi Anna Bayi na
mbele ya wanamichezo hao.
Mama
Pinda alisema wamebakiza kiasi cha sh. milioni 27 tu ambazo ni ahadi na
kwamba kama zote zitatimizwa wiki hii, hakutakuwa na taabu ya
kufanikisha mashindano hayo.
“Gharama
za kuwatayarisha wachezaji na kuendesha mashindano haya hapa nchini
zilikuwa jumla ya sh. 158,430,000/-. Kati ya hizo, gharama za kuwaweka
wachezaji kambini kwa matayarisho ni sh. 82,650,000/- na gharama ya
kuendesha mashindano kwa siku tano ni sh. 75,780,000/-,” alisema.
Aliwashukuru
baadhi ya wafadhili ambao walijitolea kulipia moja kwa moja gharama
zilizokuwa kwenye bajeti kama vile kulipia gharama za usafiri, uwanja wa
michezo, viatu vya michezo, mipira, jezi, track-suits na vifaa vingine.
Akitoa
mchanganuo wa fedha ambazo zimekwishapokelewa, Mama Pinda alisema: “Kwa
waliojitolea vifaa mbalimbali, hadi sasa tunakiri kupokea vitu vyenye
thamani ya sh. 53,080,000/- na wale waliojitolea kwa fedha taslimu
tumeshapokea jumla ya sh. 77,800,000/-. Vilevile, tunazo ahadi zenye
thamani ya sh. 27,550,000/-. Kwa kifupi hali ya kifedha kwa sasa si
mbaya kwani tunaamini walioahidi watatimiza ahadi zao ndani ya wiki hii
kabla mashindano hayajaanza”.
Mapema,
katika risala yao, wachezaji hao walisema wanakabiliwa na uhaba wa
vifaa vya mbalimbalim kama vile raba, kamba za kuruka, mipira na chupa
maalum za maji. Timu ya Taifa Queens ambayo ina wachezaji 16 na maafisa
sita, inatarajiwa kuhitimisha kambi Mei 6, 2012 na Mei 7, 2012 itahamia
jijini Dar es Salaam ili kushiriki mashindano hayo.
Baadhi
ya wake wa viongozi walioambatana na Mama Tunu Pinda ni Wake wa Makamu
wa Rais, Bi Zakia na Bi Asha Bilal, Mama Anna Mkapa, Mama Husana Kawawa,
Mama Regina Lowassa, Mama Sophia Mukama, Mama Janet Magufuli, Mama
Josephine Makamba, na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Iwezeshe Taifa
Queens Ishinde.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)